Chalamila asisitiza kuhakiki taarifa uchaguzi mkuu

DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila amewasisitiza viongozi na wananchi wa mkoa huo kuendelea kuhuisha taarifa zao ili kuweza kushiriki uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.
Chalamila ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akiwakabidhi magari katibu Tawala wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambapo amewataka kutumia magari hayo katika kutoa huduma kwa wananchi ili kutatua changamoto zao.
Aidha, pia amewataka viongozi kuendelea kuhamasisha wananchi kuhuisha taarifa zao kwa siku zilozobakia leo
“Magari haya yametolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ikiwa ni mkakati wa kuendana na Dira ya maendeleo ya Taifa hivyo amewataka viongozi wote waliokabidhiwa magari kufanya kazi ya kuwatumikia watanzania kwa uadilifu ili kubadili hali zao za maisha na kutatua changamoto zao.
Chalamila amemshukuru Rais Samia kwa kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika mwaka huu wa fedha kutokana na uhitaji Mkubwa wa ofisi hiyo ambayo kwa sasa iko pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ilala.
Kwa upande wa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, Laurance Malangwa amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa magari hayo yatakwenda kutumika kwa kuzingatia taratibu za kisheria za serikali ili yaweze kudumu na kuhudumu kwa muda mrefu .
Mkuu wa Wilaya ya Ilala,Edward Mpogolo ameahidi kuwahudumia kwa karibu wananchi ili kutatua kero zao na kuwakumbusha suala la kuhuisha taarifa zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka huu.