DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanadumisha amani na utulivu, akisema kuwa ni nguzo muhimu katika ustawi wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kutembelea soko la Temeke Stereo na kituo cha daladala cha Buza wilayani Temeke, Chalamila amesema kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi, hivyo ni muhimu kuepuka vikundi vyenye nia ya kutumia siasa kuchochea uvunjifu wa amani.
“Amani ikipotea, shughuli zote za kiuchumi na kijamii haziwezi kufanyika. Ni wajibu wetu sote kulinda utulivu wa nchi kwa faida ya maendeleo ya Taifa,” amesema Chalamila.
Aidha, amewahimiza wafanyabiashara kulipa kodi stahiki akibainisha kuwa kodi ni msingi wa maendeleo kwa taifa, huku akiwataka kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanachangia ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Katika kituo cha daladala cha Buza, ambacho hakitumiki ipasavyo licha ya kujengwa na serikali, Chalamila amewataka watendaji wa wilaya kuhakikisha magari yote yanapaki ndani ya kituo badala ya kuendelea kupaki barabarani. Amesisitiza pia umuhimu wa biashara kufanyika saa 24 ili kuongeza tija ya kiuchumi.
Akiwa katika soko la Temeke Stereo, Chalamila alipokea kero mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara, zikiwemo miundombinu mibovu, ukosefu wa vivuli, na biashara kufanyika barabarani. Ameagiza Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Jomari Mrisho Satura, kushughulikia changamoto hizo.
Kwa upande wake, Mapunda na Satura waliahidi kutatua changamoto hizo na kusimamia utekelezaji wa mpango wa kufanya biashara saa 24 kwa kuhakikisha miundombinu ya taa inaboreshwa.
Chalamila amehitimisha ziara yake kwa kufanya mkutano wa hadhara katika kituo cha polisi cha Tandika, ambako amesisitiza msimamo wa mkoa huo kuhusu biashara saa 24, kudumisha amani, na kulipa kodi stahiki kwa maendeleo ya taifa.