Chalamila ataka miradi Ubungo ikamilike kwa wakati

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Ubungo na kutoa agizo kwa wasimamizi kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati ili iwe na viwango stahiki.

Akizungumza baada ya kuweka Jiwe la Msingi katika ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Mpiji Magoe, Chalamila amesema serikali inalenga kuona miradi ya afya inasaidia kutatua changamoto zinazowakabili akina mama na watoto.

“Lazima miradi hii iwe imara na idumu kwa miaka mingi, kwa sababu tunatumia fedha za wananchi. Hatuwezi kukubali ujenzi usio na viwango,” amesema Chalamila.

Katika hatua nyingine, alipofika katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Goba Kulangwa, mkuu huyo wa mkoa alisisitiza umuhimu wa usalama hasa kuelekea uchaguzi mkuu na kuagiza kukamilishwa haraka kwa ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Tegeta A.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Juma Japhari Nyaigesha, aliwataka wananchi na wafanyabiashara kutokwepa kulipa kodi kwa kuwa ndicho chanzo kikuu cha fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Kodi zetu ndizo zinazojenga vituo vya afya kama hiki cha Mpiji Magoe. Wananchi tushirikiane kuiunga mkono serikali,” amesema Meya Nyaigesha.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mpiji Magoe, Hereswida Cosmas, alieleza kuwa ujenzi wa jengo la mama na mtoto umefikia hatua nzuri na linatarajiwa kusaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa hususan wanawake wajawazito.

Katika ziara hiyo, Chalamila pia alikagua mradi wa maji wa Kibamba na kujionea maendeleo ya miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button