Chalamila atoa maagizo wa DC ubovu wa barabara Msongola

DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila ameitaka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala kushughulikia changamoto ya ubovu wa barabara za Kata ya Msongola iliyopo ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam mara baada ya mvua kupungua.

Chalamila ameagiza hayo leo katika ziara ya maeneo ya miradi ya kiserikali inayoendelea kujengwa katika Kata ya Msongola, Kata ya Chanika na Kata ya Zingiziwa  ikiwemo ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Kata ya Msongola  na ujenzi wa Zahanati ya Nzasa, jijini humo.

“Nimesikia na kujionea changamoto ya barabara ni kweli barabara hazipitiki sasa naelekeza ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Ilala mvua zikipungua ni kuangalia mguu kwa mguu athari zilizosababishwa na mvua ili tutakapoenda kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati miradi hiyo tuwe na uwakika hata mvua ikija miradi hiyo haitaathirika tena na mvua kuliko kukimbilia kufanya ukarabati wa muda mfupi mfupi wakati huu mvua zikiwa zinanyesha tunaweza tukakarabati lakini hakuwezi kuwa na ubora kama tukisubiri mvua zipungue,” amesema Chalamila.

Kwa upande mwingine, Chalamila amempongeza Mkuu wa Shule ya Sekondari Mvuti kwa usimamizi mzuri wa shule mpya ya sekondari inayojengwa ndani ya Kata ya Msongola, kwa thamani ya Sh 528,998,424.

“Nimekuja nikifuatilia ujenzi wa shule hii na kujionea jinsi ulivyojengwa kwa ubora wa hali ya juu kutokana na fedha zilizotolewa na serikali,” amesema mkuu huyo.

Hata hivyo, Chalamila ametembelea Zahanati ya Nzasa inayojengwa katika Kata ya Zingiziwa kwa takribani Sh milioni 150, ifanyiwe marekebisho ikiwemo kutengeneza njia za chemchem katika eneo hilo ili ianze kutumika haraka iwezekanavyo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wakandarasi na wasimamizi wengine wa miradi ya Shule kuiga mfano wa shule hiyo iliyojengwa kwa kisasa ambayo madarasa yake yamejengwa kwa marumaru, umeme na madirisha yenye vioo vya alminiamu pamoja na kuwa na maabara za kisasa za kujifunza.

“Nikupongeze Mkuu wa shule kwa kujenga shule za kisasa ikiwemo kuweka marumaru kwa sababu mara nyingi shule nyingi wamekuwa zikiathirika pindi sakafu ikiharibika wanafunzi wanakaa kwenye vumbi naomba hata watu wengine wanaokarabati au kujenga shule waige mfano huu kwasababu wapi Wakuu wa shule nyingine wamepewa fedha kama mlizopewa ninyi lakini ila wameshindwa kuweka hata marumaru na umeme kwenye madarasa,” amesema Mpogolo.

Amesema mradi wa shule hiyo umegharimu Sh milioni 528 hata hivyo halmashauri ya Jiji hilo imetoa Sh milioni 200 kwa ajili ya Ujenzi wa darasa la kujifunzia somo la Jografia.

Mpogolo amesema pia halmashauri hiyo imetoa Sh milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa shule ya sekondari ya zamani ya Mvuti ili hata wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wasome katika mazingira rafiki na salama.

Habari Zifananazo

Back to top button