Chalamila atoa maelekezo uchaguzi mitaa

DAR ES SALAAM: Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limetakiwa kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, unakuwa huru na haki wakishirikiana na wizara yenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Maelekezo hayo yametolewa Dar es Salamm leo Oktoba 7, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Albert Chalamila wakati akikabidhi pikipiki kwa Jeshi la Polisi, Zimamoto, Uhamiaji na Magereza na kusisitiza kuwa usalama wa uchaguzi ni kipengele muhimu cha kudumisha demokrasia nchini.

Amesema jeshi hilo lina jukumu la kushirikiana na wadau wanaosimamia uchaguzi na vyombo vingine kuhakikisha wananchi wanapiga kura kwa uhuru bila hofu yoyote.

Advertisement

Isome pia: Takukuru kutoa elimu ya rushwa uchaguzi mitaa

“Usalama wa uchaguzi ni muhimu ili wananchi wawe na imani na viongozi watakaochaguliwa, mashaka yoyote kuhusu uadilifu wa uchaguzi yanaweza kuathiri utulivu wa taifa,” amesema Chalamila.

RC Chalamila

Aidha, Chalamila amezungumzia umuhimu wa kulinda usalama wa viongozi wa kitaifa, hususan Rais, ambaye amebeba dira ya taifa na kuongeza kuwa kuna vikundi ambavyo vina nia mbaya ya kuhatarisha amani ya taifa, lakini Jeshi la Polisi limekuwa likidhibiti hali hiyo kwa ufanisi.

“Amani ya nchi yetu lazima idumishwe kwa gharama yoyote, na jeshi letu limeonesha uwezo huo.” amesema.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameeleza kuwa vyombo hivyo vya usafiri vitasaidia kuboresha operesheni za kudhibiti uhalifu na kuimarisha usalama, hususan kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

“Tutaendelea kufanya kazi zetu kwa mujibu wa katiba, kuhakikisha usalama jijini Dar es Salaam na kuruhusu shughuli za kiuchumi kuendelea kwa utulivu,” amesema.