Chalamila awaonya mabaunsa Dar

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kufuatia ukiukwaji wa sheria na vitendo vya ukatili vilivyofanywa na mabaunsa dhidi ya wapangaji wa Alice Paskali Haule kwenye nyumba yenye mgogoro iliyopo Msasani Beach jijini Dar es Salaam, ameagiza kuanzia sasa mabaunsa wasitumike kutoa watu kwenye maeneo yenye migogoro badala yake madalali wa mahakama watumie jeshi la polisi ambao wanaweledi wa kufanya kazi hiyo

Mgogoro wa nyumba hiyo ambayo ni kiwanja namba 891 inahusisha mke wa marehemu Justis Lugaibula, Alice Paskali Haule na bwana Muhamed Mustafa Yusufali ambaye anaonekana alinunua nyumba hiyo kutoka kwa marehemu Justis Lugaibula enzi za uhai wake bila kumshirikisha mkewe

Akizungumza jijini Dar es Salaam RC Chalamila ametoa agizo hilo leo septemba 24 alipofika katika nyumba hiyo Msasani Beach jijini humo baada ya Septemba 23 kuona ‘video’ zikionesha mabaunsa wakitumia nguvu kubwa na ukiukwaji wa haki za binadamu kuwaondosha watu waishio kwenye nyumba hiyo yenye mgogoro.

Aidha, Chalamila ameagiza nyumba hiyo kutotumika na upande wowote wa mgogoro hadi hapo mgogoro utakapomalizika ambapo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuunda kamati ya wataalamu ikiwemo jeshi la polisi, ofisi ya kamishina wa ardhi na wataalamu wengine ambapo ameitaka kamati hiyo na pande zote mbili za mgogoro kufika ofisini kwake Ijumaa Septemba 26

Hata hivyo akizungumzia mgogoro huo, Alice Pascal Haule ambaye ni mke wa marehemu Justis Lugaibula amesema yeye na mumewe walinunua nyumba hiyo mwaka 2008 lakini amekuwa akipata usumbufu kutoka mabaunsa wakidai kuwa Muhamed Mustafa Yusufali aliuziwa nyumba hiyo na mumewe wakati yeye anafahamu walikopeshana pesa na sio kuuziwa nyumba.

Naye mwakilishi wa Muhamed Mustafa Yusufali ambaye yupo safarini, Hajja Mungula amesema yeye anafahamu kuwa Muhamed alinunua nyumba hiyo mwaka 2011 kutoka kwa Marehemu Justis Lugaibula ambaye ni mume wa Alice kwa shilingi milioni 262 na kwamba Alice aliweka alama yake ya dole gumba kwenye nyaraka ya mauziano

Kwa upande wa Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukrani Kyando ameeleza namna ambavyo nyaraka za nyumba hiyo zilivyokuwa zikibadilishwa kila inapouzwa na kusema kuwa kwa mujibu wa nyaraka zilizopo sasa nyumba hiyo aliuziwa Muhamed Mutafa Yusufali na hivyo hati inasoma jina lake huku mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule akisisitiza changamoto ya uwepo wa mabaunsa wasio na weledi wa kazi katika wilaya hiyo

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button