Chalinze, Handeni mambo yaiva mradi wa maji

Chalinze, Handeni mambo yaiva mradi wa maji

TAKRIBANI wakazi 200,000 wa Halmashauri za Chalinze, Handeni na baadhi ya vijiji vya Morogoro, wanatarajiwa kuanza kunufaika na huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa mradi wa Chalinze Awamu ya Tatu unaotarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi ujao.

Akizungumza maendeleo ya mradi huo leo Januari 17, 2023, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema kuwa mradi umetekelezwa kikamilifu kwa asilimia 96 mpaka sasa, na kufikia mwishoni mwa Februari utakuwa umekamilika.

Amesema tayari ujenzi wa matenki 18 ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 500,000 mpaka milioni 2 umekamilika.

Advertisement

Pia amesema kati ya vituo vya kusukuma maji 10 vinavyojengwa, vituo saba vimekamilika, ujenzi wa mtandao wa kusafirisha maji kwa umbali wa kilomita 1,268 pamoja na ujenzi wa vizimba vya kuchotea maji 351, ambavyo vyote vimekamilika.

“Mpaka sasa utekelezaji umeenda vizuri na kazi kubwa imefanyika ndani ya muda uliopangwa, kazi iliyobaki kwa sasa ni kufunga pampu kwenye mtambo wa maji Wami. Pampu zimeshafika hivyo ni suala la kufunga tu,” amesema Luhemeja.