CHAN imeisha, tujipange kwa michuano mingine

SAFARI ya Taifa Stars kwenye michuano ya Mabingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) imeishia kwenye hatua ya robo fainali baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Morocco.
Robo fainali ni hatua ya juu kufikiwa na Stars katika michuano hiyo ambayo ilifanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu za Afrika Mashariki: Tanzania, Kenya na Uganda. Stars ilipangwa Kundi B, pamoja na nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mauritania, Burkina Faso na Madagascar.
Wenyeji Stars walimaliza nafasi ya kwanza katika kundi hilo, wakikusanya pointi 10 baada ya kushinda michezo mitatu na kupata sare kwenye mchezo mmoja, walifanikiwa kufunga mabao matano na kuruhusu bao moja pekee.
Hii ni mara ya tatu kwa Stars kushiriki kwenye michuano hiyo, mara ya kwanza kushiriki ilikuwa michuano ya 2019 na mara ya pili ni 2022. Katika awamu zote mbili za mwanzo, Stars haikufanikiwa kuvuka hatua ya makundi, mashindano ya awamu hii Stars imeweka rekodi mpya.
soma: Taifa Stars yaanza kwa kishindo CHAN
Swali kubwa linalobaki kwa wapenda soka nchini Je, baada ya kiwango kizuri kilichooneshwa na Stars kwenye michuano hii, nini kifanyike kwa ajili michuano mingine iliyopo mbeleni?
Baada ya timu kuondoshwa kwenye mashindano, Kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema wataitumia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi ya michuano mingine ikiwemo Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).
“Tunajivunia jitihada za wachezaji wangu ambao walicheza kwa moyo wote. Ingawa hatukufanikisha kufuzu nusu fainali, nina imani hii ni hatua nzuri katika maendeleo yetu ya soka kama nchi,” alisema Morocco.
Aliongezea kuwa: “Tunahitaji kuendelea kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza kama suala la washambuliaji kupoteza nafasi, tutaandaa mifumo mizuri ya kuwaandaa washambuliaji wetu vyema. Naelewa nchi yetu ina uhaba wa washambuliaji, imekuwa ni kama ugonjwa wa taifa.”
Aliongezea kuwa nchi ina uhaba wa wachezaji wengi kwenye nafasi ya ushambuliaji na ndiyo maana timu kubwa za Tanzania (Simba, Yanga na Azam) zinatumia wachezaji wengi wa kigeni kwenye eneo hilo. Alisema kupitia michuano hii Stars imejipambanua kama sio tu timu shiriki, bali timu shindani.
“Nashukuru wadau na mashabiki wote wa soka nchini kwa sapoti yao. Tutaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha Taifa Stars inazidi kuwa timu shindani Afrika,” alisema Morocco. Kitu kingine ambacho Morocco alisisitiza ni wachezaji kufanya vizuri kwenye timu zao, ili timu ya taifa iwe na kikosi kipana zaidi.
“Tutarudi kwenye uwanja wa mazoezi lakini pia wachezaji wanatakiwa kufanya vizuri kwenye timu zao,” alisema Morocco. Pia, alisisitiza suala la timu kupata mechi nyingi za kirafiki ili kujenga uwiano mzuri wa wachezaji.
Naye Kocha msaidizi wa Stars, Juma Mgunda alisema michuano hiyo imewapa funzo kubwa kwa hiyo watajua pa kuendelea ili timu ifanye vizuri zaidi.
“Kwanza tunawashukuru vijana wetu, wamepambana na tumefikia hatua nzuri inayoonesha kuwa inawezekana. Kikubwa tumeshajua wapi tulifika, tutaendelea tulipoishia kwenye michuano mingine tukianza na mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Jamhuri ya Congo Septemba 5,” anasema Mgunda.
Kwa upande wa mamlaka za mpira nchini, ni lazima timu ya taifa ihakikishiwe yanaandaliwa mazingira mazuri, ikiwemo kuandaa sera nzuri za michezo hasa kuvilazimisha vilabu vikubwa vya Simba na Yanga vitoe fursa kwa vijana wa Tanzania wenye vipaji kushiriki kwenye michuano mikubwa ili wapate uzoefu wa mashindano makubwa Afrika.
Simba na Yanga ziache mara moja mazoea ya kuwakusanya wachezaji wengi wenye vipaji wanaokosa nafasi ya kucheza na kuishia kukaa benchi tu. Mamlaka za soka zihakikishe timu ya taifa inatafutiwa mechi nyingi za kirafiki zenye uzito wa juu ili timu ijiandae vizuri kuelekea kwenye mashindano mbalimbali.
Lakini pia, kikosi cha timu ya taifa kiitwe kwa kuzingatia ubora wa mchezaji aliouonesha na sio kuangalia majina na timu anayotoka. Wapenzi wa soka nchini wanasisitiza kuwa licha ya mafanikio haya, Tanzania inahitaji kuwekeza zaidi katika maendeleo ya wachezaji wa ndani.
Kuendeleza vipaji vya vijana ni hatua muhimu zitakazowasaidia Taifa Stars kufikia mafanikio makubwa katika michuano ya kimataifa.



