DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Habari na Mawasiliano, Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka Watanzania kuchangamkia huduma za mawasiliano zinazotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) zilizosambaa maeneo mbalimbali nchini ikiwemo maeneo ya pembezoni.
Mahundi, ametoa wito huo alipofanya ziara ya kikazi ofisi za makao makuu ya shirika hilo Posta, jijini Dar es Salaam, kujionea huduma za mawasiliano zinazotolewa na shirika hilo.

“Huduma zinazotolewa na TTCL zinaboresha huduma za mawasiliano maeneo ya pembezoni, ikizingatia zaidi utoaji wa huduma za mawasiliano kwa jamii badala la kufanya biashara na kutengeneza faida,” amesema.
Naibu Waziri huyo amesema serikali imeendelea kuiwezesha TTCL kutoa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi ikiwemo kusaini mkataba wa kujenga minara 636 itakayowezesha kuyafikia maeneo ya pembezoni, na kutatua changamoto ya mawasiliano katika maeneo hayo.

Mha. Mahundi amebainisha kuwa TTCL hainabudi kujivunia ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano unaotoa huduma kwa nchi sita za Africa, zinazotegemea mawasiliano kupitia mkongo huo.
Amefafanua kuwa ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano umefungua fursa za utoaji wa huduma ya mawasiliano na kuwataka TTCL kuendelea kuboresha huduma zao katika kuthamini jitihada na maono ya Serikali katika kuimarisha huduma za mawasiliano kwa jamii.

Kwaupande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA. Moremi Marwa amesema Shirika linatoa huduma na kuziboresha ikiwemo huduma ya kifedha na data na kuwataka wateja wa TTCL kuendelea kuliamini Shirika kwa kutumia huduma zake.
Ziara hiyo ya kikazi ni mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha katika taasisi mbalimbali za mawasiliano, kuona na kupata uwelewa zaidi katika kutimiza majukumu ya shirika hilo kwa upande wa mawasiliano.