BIASHARA Ndogo na za Kati (SMEs) ndiyo moyo wa uchumi wa nchi kwa kuwa hufanya kazi kama kichocheo cha ukuaji, uvumbuzi na fursa za kiuchumi.
Biashara hizi huchangia katika Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 35 na kuajiri watu wengi na hivyo kudhihirisha umuhimu wake kwa ustawi wa taifa.
Mbali na kuchochea maendeleo haya ya kiuchumi, biashara ndogo na za kati hubadili maisha ya watu kwa kuondoa au kupunguza umasikini na kuinua jamii kupitia ubia wa ujasiriamali.
Kimsingi, hujumuisha uhimilivu na mabadiliko kuakisi mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini. Mjadala huu unajikita katika mazingira tata ya kodi yanayodaiwa kuzikabili SMEs Tanzania.
Unalenga pia, kutazama changamoto na fursa mbalimbali katika mfumo wa kodi nchini ukibainisha namna
changamoto na fursa hizo zinavyoathiri ukuaji na uendelevu wa biashara hizo. Uelewa sahihi na wa kutosha kuhusu mienendo hii utawezesha watunga sera, wadau na wajasiriamali kushirikiana kujenga mazingira wezeshi na rafiki zaidi kwa SMEs kustawi.
Uchanganuzi huu unaegemea katika mbinu thabiti zinazojumuisha visa mikasa (mifano), tafiti pamoja na mahojiano na wamiliki wa biashara ndogo na kati kuonesha hali halisi ya biashara zinazotumia mfumo wa kodi.
Mapitio ya Sera
Mshauri wa masuala ya kodi nchini, Simbawene Kitalu anasema kupitia sera za kimaendeleo, Tanzania imepiga hatua kubwa kuchochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati. “Sera ya Taifa ya Maendeleo ya SMEs ya Mwaka 2003 inatumika kama nguzo ya ukuaji wa biashara ndogo na za kati kwa kutatua changamoto za upatikanaji wa
fedha, teknolojia na masoko,” anasema.
Anaongeza: “Sera hii imefanikiwa kuziba pengo la upatikanaji wa fedha na kuongeza kiwango cha biashara ndogo
na za kati zinazopata huduma za mikopo kutoka asilimia 20 hadi zaidi ya asilimia 40”.
“Tangu kuanza kutekelezwa kwake, sera hiyo inahimiza mipango ya uhamishaji wa teknolojia na kuwezesha biashara takribani 30,000 kupata nyenzo na mbinu za kisasa,” anafafanua.
Mtaalamu mwingine katika masuala ya kodi, Yudathadey Kavishe anasisitiza urasimishaji kama nguzo muhimu kwa ukuaji wa biashara ndogo na za kati. “Biashara rasmi huchangia takribani asilimia 70 zaidi katika mapato ya kodi ikilinganishwa na biashara zisizo rasmi,” anadokeza.
Katika kuchochea mabadiliko haya, Kavishe anasisitiza hatua kadhaa za serikali zikiwamo kurahisisha mchakato wa usajili wa biashara, kupunguza muda kutoka siku 30 hadi chini ya siku saba na kuanzisha kampeni za uhamasishaji wa umma nchini.
Anasema, “Kampeni hizi zimefikia zaidi ya biashara milioni moja zisizo rasmi na kuhamasisha urasimishaji wa
shughuli hizo na kuunganishwa katika uchumi rasmi.” Maoni hayo yanatoa taswira ya kuvutia kuhusu Tanzania
inavyoweka mazingira wezeshi kwa biashara ndogo na za kati kustawi.
Mmoja wa watendaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Mwanza ambaye jina lake halikupatikana mara moja,
anazungumzia umuhimu wa mipango kama vile Mpango wa Udhamini wa Mikopo wa Biashara Ndogo na za Kati
(SME-CGS) katika kukuza upatikanaji wa kifedha kwa biashara ndogo na za kati.
Anasema kwa kiasi kikubwa, mpango huu hupunguza hatari zinazoletwa na taasisi za fedha na kuzihimiza kuongeza
mikopo yenye riba na masharti nafuu ili kuwezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kumudu.
Aidha, serikali hushirikiana kikamilifu na benki na taasisi ndogo za fedha kutengeneza bidhaa bora za kifedha zinazokidhi changamoto za kipekee zinazokabili biashara hizo.
Mbali na kuwezesha upatikanaji huo wa mikopo, pia zinatekelezwa programu za kujenga uwezo ili kuwapa ujuzi muhimu wamiliki wa biashara katika usimamizi wa fedha, ujasiriamali na kupata teknolojia. Kwa pamoja, juhudi hizi hukuza ushindani na uhimilivu wa biashara katika hali ya soko inayobadilika.
Mapitio ya mfumo wa kodi
Hali na mazingira ya kodi kwa biashara ndogo na za kati nchini inasimamiwa na sera mbalimbali zinazosaidia utekelezaji wa sheria za kodi. Sera hizo muhimu za kodi ni pamoja na mfumo wa makadirio ya kodi, muundo wa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya 2015, ambazo zote hurahisisha masuala ya kodi kwa biashara.
Mshauri wa masuala ya kodi, Lisa Kileghe alinukuliwa katika mahojiano akizungumzia mfumo wa makadirio ya kodi unavyosaidia biashara ndogo na za kati kwa mauzo ya kila mwaka chini ya Sh milioni 100 kwa kutoa muundo wa ngazi unaopunguza matatizo ya kiusimamizi.
Anasema mfumo wa VAT unataka biashara zenye mauzo ya zaidi ya Sh milioni 100 kuchangia mapato ya umma kupitia kiwango cha kawaida cha asilimia 18.
Kileghe anasisitiza kwamba Sheria ya Usimamizi wa Kodi husaidia mifumo hii kwa kuzipa biashara ndogo na za kati miongozo ya namna ya kutekeleza sheria za kodi, kutatua mizozo na adhabu ili kujenga mazingira ya kodi yenye uwazi na yanayotabirika.
Mmoja wa wachumi anayeishi Shinyanga, Seleman Issa anasema mahitaji muhimu ya utekelezaji wa sheria za kodi huwekwa kwa uangalifu kadiri ya makundi tofauti ya mauzo na hivyo kuleta uwiano kati ya udhibiti na ukuaji wa
biashara.
Kwa mujibu wa Issa, biashara zinazopata chini ya Sh milioni nne kwa mwaka hazihusiki na kodi ya mapato huku za kundi la juu yake hufuata kanuni maalumu kwa kadiri ya mauzo. Anadokeza kuwa usajili wa VAT unahusisha pia,
matumizi ya lazima ya vifaa vya kifedha vya kielektroniki (EFDs) ili kuimarisha usahihi na uwajibikaji.
Issa anasema hatua hizi za pamoja zinaonesha dhamira ya dhati ya serikali kujenga mfumo wa kodi ambao si tu
kwamba unasaidia ukuaji wa biashara, bali pia unahakikisha kunakuwapo utekelezaji wa sheria za kodi na udhibiti.
Kuthibitisha athari za uboreshaji huu, utafiti wa hivi karibuni ulibainisha kisa cha duka dogo la rejareja la Kazi Bora Traders jijini Arusha.
Kabla ya duka hilo kujiandikisha katika mfumo wa makadirio ya kodi, biashara zilikuwa zikikumbana na ugumu katika uwasilishaji wa taarifa za kodi uliozuia ukuaji. Kwa kutumia mfumo uliorahisishwa, duka hilo lilirahisisha utekelezaji wa majukumu yake ya kodi na kupunguza gharama za usimamizi kwa asilimia 30.
Hili lilimwezesha mmiliki kutumia muda na rasilimali nyingi katika uendeshaji na matokeo yake yamekuwa kuongezeka kwa asilimia 15 ya mauzo kwa mwaka. Pamoja na mafanikio haya, mmiliki huyo alikiri kuwapo changamoto kadhaa, zikiwamo za ujuzi mdogo wa kidijiti ambao mara kwa mara ulikuwa ukizuia matumizi bora ya mifumo ya kodi ya kielektroniki.
Mifano hiyo inaonesha umuhimu wa kurahisisha mchakato wa kutekeleza sheria za kodi na kufanya juhudi za
makusudi kuzijengea uwezo biashara lengwa. Ushuru wa bidhaa na kodi ya zuio hutumika katika sekta mahususi kama viwanda na ujenzi. Kodi katika sekta hizi hukadiriwa kwa kuzingatia asili ya bidhaa au huduma zinazotolewa.
Kwa biashara zinazohusisha kuvuka mipaka ya nchi, ushuru wa forodha na kodi inayotozwa kwa bidhaa au huduma zinapovuka mpaka au kuingiza kwenye soko la ndani husimamiwa na Ushuru wa Pamoja wa Nje wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhakikisha kunakuwapo usawa ili kupunguza vikwazo vya biashara katika kanda.
Mtafiti wa kujitegemea anayeishi Dar es Salaam ambaye ni mhitimu wa Shule ya Biashara ya Wits, Penelope Mhandiki anajadili hatua kubwa zilizopigwa katika kutekeleza sheria za kodi kwa biashara ndogo na za kati katika miaka ya karibuni.
“Kati ya mwaka 2015 na 2023, viwango vya utekelezaji sheria za kodi ya VAT viliongezeka kutoka asilimia 65 hadi 78 kutokana na ubunifu wa kidijiti kama vile Mfumo wa Usimamizi wa Kodi Kielektroniki (ETMS) na kampeni za elimu zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” anasema.
Kwa mujibu wa ripoti za TRA, hadi mwaka 2022, zaidi ya biashara 50,000 zilikuwa zimeandikishwa katika ETMS na kusababisha punguzo la asilimia 20 la makosa ya uwasilishaji wa taarifa za kodi. Matumizi ya EFD yameboresha kwa kiasi kikubwa uwazi na uwajibikaji na hadi kufikia 2023, zaidi ya mashine za EFD 90,000 zimesambazwa kwa biashara mbalimbali nchini.
Joyce Kachema kutoka Kachema Associates anasema, “Takwimu hizi zinadhihirisha namna hatua hizi zilivyosaidia
kupunguza ukwepaji wa kodi kwa takribani asilimia 25 katika sekta muhimu kama vile biashara za rejareja na viwanda na hata kuchangia Shilingi bilioni 300 kwenye mapato ya kodi kwa mwaka.”
Pamoja na mafanikio hayo, wataalamu hao wanasisitiza kuwa bado kuna changamoto kadhaa hususani katika kufikia biashara ndogo na za kati vijijini ambako uelewa wa nyenzo za kutekeleza masuala ya kodi ni mdogo na gharama za uendeshaji kwa kutumia nyenzo hizo ni kubwa.
Mambo haya yanayoendelea yanaonesha umuhimu wa uboreshaji kujenga mazingira jumuishi zaidi ya kodi kwa biashara ndogo na za kati nchini.
Upatikanaji soko na mifumo ya udhibiti
Katika mjadala kuhusu mikakati ya upatikanaji wa soko la Tanzania, wataalamu wa manunuzi, James Kirika, Juma Pendaeli, Juliana Peter na David Mosha wanakiri serikali imetekeleza mipango na sera zenye matokeo chanya
zinazoweka kipaumbele katika biashara ndogo na za kwa manunuzi ya ndani.
Mtaalamu katika manunuzi, vifaa na usimamizi wa ugavi, James Kirika alijikita katika kanuni za ushiriki wa wazawa katika Sheria ya Manunuzi ya Umma inayoelekeza biashara ndogo na za kati kupata walau asilimia 25 ya kandarasi za serikali.
“Sera hii imeelekeza zaidi ya Sh trilioni 1.2 kila mwaka kwa biashara ndogo na za kati tangu mwaka 2020 na hivyo, kutengeneza fursa muhimu kwa biashara za ndani,” anasema. Wataalamu hao wanasisitiza umuhimu wa majukwaa mbalimbali, yakiwamo Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayovutia washiriki zaidi ya 500,000 kutoka zaidi ya nchi 30 kila mwaka.
“Maonesho haya huwezesha mikataba ya takribani Shilingi bilioni 200 kila mwaka kusaidia SMEs kupanua wigo na vyanzo vya mapato,” anasema Juliana Peter.
Harakati zinazofadhiliwa na serikali, ukiwamo Mpango wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo ya Nje (ECGS) pia, zilipongezwa kwa kuongeza zaidi ya Sh bilioni 50 katika dhamana ya mikopo kwa biashara tangu kuanzishwa na hivyo kuwezesha upatikanaji wa masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Juma Pendaeli anasisitiza umuhimu wa ushirikiano na taasisi za kikanda kama Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC). “Ushirikiano huu umeongeza fursa za biashara za mipakani huku biashara ndogo na za kati zikichangia zaidi ya asilimia 15 katika biashara ya ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ifikapo 2023,” anasema.
Wataalamu hao wanasema mipango hii si tu kwamba inaleta vyanzo mbalimbali vya mapato kwa biashara, bali pia
inahimiza uvumbuzi na uimarishaji wa ubora wa bidhaa kufikia viwango vya kimataifa. Mifumo ya udhibiti imerahisishwa ili kujenga mazingira rafiki zaidi ya kufanya biashara nchini.
Kwa mfano, kuanzishwa kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kumeweka urahisi kwa wajasiriamali kusajili biashara zao kimtandao na hivyo kupunguza muda wa usajili hadi siku tatu.
Mbali na hayo, serikali imeanzisha Sheria ya Ushindani wa Haki inayolenga pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kunakuwapo ushindani wa haki na usawa katika soko.
Sheria ya Uwekezaji Tanzania ni mfano mwingine unaotoa motisha na ulinzi kwa biashara zinazowekeza katika sekta za kipaumbele kama kilimo na nishati jadidifu. Kwa pamoja, mifumo hii inalenga kupunguza vikwazo vya ukiritimba, kukuza uwazi na kuweka usawa kwa biashara kustawi katika uchumi shindani.
Hitimisho
Kupitia utekelezaji wa sera hizi, Tanzania inajenga na kukuza mfumo wa ikolojia ambao biashara zinaweza kustawi
kwa kushughulikia changamoto za kipekee na kuifungua katika ukuaji.
Juhudi za kimkakati katika maboresho ya kodi, kujenga uwezo na kuongeza ubora katika udhibiti si tu kwamba
hurahisisha mchakato wa biashara, bali pia huwezesha biashara ndogo na za kati kutoa mchango mkubwa kwa Pato la Taifa, kuunda fursa za ajira na kushindana ipasavyo katika kiwango cha kimataifa.
Juhudi hizi ni mfano wa maono ya Tanzania kuanzisha biashara ndogo na za kati kama injini ya maendeleo ya
kiuchumi na nguzo za maendeleo shirikishi kuhakikisha kuna uthabiti na ustawi wa muda mrefu.