PWANI; Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme wa Msongo wa kilovoti 400/220/132/33 wa kituo cha Chalinze umefikia asilimia 84.3 na hivyo kuleta matumaini ya kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme.
–
Hayo yameelezwa leo Oktoba 12, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko alipotembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa kituo hicho cha Chalinze Mkoani Pwani, kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
–
“kwa sasa ujenzi umefikia asilimia. 84.3 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 31 Disemba, 2023. Mradi huu unakwenda kupunguza changamoto ya umeme kwa kiasi kikubwa hususan katika mkoa huu wa Pwani,” amesema Dkt. Biteko.
–
Ameongeza kuwa, mara baada ya Mradi huo kukamilika, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea Megawatt 2115 kutoka katika Bwawa la kuzalisha Umeme wa Maji la Julius Nyerere na kitasambaza Megawati 850 kwenye mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani na kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika mikoa hiyo.
–
Naye, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kuwa, Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa mradi utakapokamilika utakua ni msaada mkubwa wa mkoa wa Pwani.
–
Mradi huo ulianza rasmi tarehe 6 Septemba, 2021 ambapo kazi za ujenzi zilianza tarehe 11 Oktoba, 2021 na unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze pamoja na ituo cha kupoza umeme na kusafirisha umeme kuelekea mikoa ya kaskazini kwa kuingizwa Kenya Gridi ya Taifa.
Imeandaliwa na Mwandishi Wetu.
–
una maoni usisite kutuandikia