Chanzo migogoro wafugaji, wakulima kuchukuliwa hatua

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imelitaka jeshi la polisi mikoa ya Lindi na Mtwara kuwabaini na kuwachukulia hatua vinara wa migogoro kati ya wakulima na wafungaji katika mikoa hiyo.

Sambamba na hilo, wizara hiyo imewataka wasimamizi wa sheria kusimamia sheria na mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafungaji.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ametoa maagizo hayo wakati akifungua maonesho ya Nanenane 2023 Kanda ya Kusini ambayo yanafanyika katika viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.

“Wasimamizi wa sheria hasa jeshi polisi kuwa imara katika kubaini na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaonekana kuwa ni vinara ya migogoro,” amesema.

Sagina amewataka pia jeshi hilo, viongozi wa vijiji, kata na wilaya kuwa imara katika kusimamia sheria na mipango ya matumizi bora ya ardhi kuepusha migogoro ya wakulima na wafungaji.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telak amesema kuwa kumekuwepo na wimbi la wafugaji ambao wanaingia na mifugo wengi kwenye mikoa hiyo kinyume na sheria na kuleta migogoro kwa wakulima.

“Wapo wafugaji ambao wanaingia kinyume na utaratibu wakiwa na makundi makubwa ya mifugo, hawa wamekuwa kero na wanasababisha adha kubwa kwa wakulima na rasilimali za wakulima,” amesema.

Telak amesema wapo watu wamepata ulemavu kwa sababu ya vipigo kutoka kwa wafungaji na wengine kupoteza maisha kwa sababu ya wafugaji.

Amesema jeshi la polisi na wasimamizi wengine wa sheria wanaendelea kuchukua hatua ikiwemo kuchukua hatua Kudhibiti migogoro hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button