Chemchemi majimoto, kivutio cha utalii Rufiji chenye maajabu yake

CHEMCHEMI ya majimoto iliyoko wilayani Rufiji mkoani Pwani ni ya kihistoria kwani iligundulika mwaka 1905 na wenyeji wanaoishi eneo hilo kabila la Wandengereko.

Wakati huo Tanzania ilikuwa chini ya koloni la Wajerumani ambapo Wandengereko walipogundua hilo walipeleka taarifa kwa watawala.

Ofisa Utalii Wilaya ya Rufiji kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Athuman Baragaza, anasema wakoloni waliingia katika eneo hilo na kulipenda kwa ajili ya kuliendeleza kwa shughuli za utalii.

“Ilipofika mwaka 1914 tuliingia Vita ya Kwanza ya Dunia mpaka 1918 ilipoisha  na Wajerumani wakaondoshwa na Waingereza katika koloni la Tanganyika. Waingereza pamoja na kupitia maeneo mengi lakini eneo la chemchemi hiyo walilipenda na kuvutiwa nalo zaidi,” anasema Baragaza.

Anasema Waingereza walifanya jitihada za kulirasimisha kuwa hifadhi mwaka 1930 na ilipofika mwaka 1945 walijenga eneo hilo kwa kuweka msingi wa mawe.

Kwa maelezo ya Baragaza, kituo hicho mwanzo kilikuwa na miti mingi kwani eneo lote lilizungukwa na miti mpaka kisima kilifunikwa kwa kuwa kivuli kilikaa kwenye eneo hilo.

“Ila uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo umesababisha eneo hilo kuwa jangwa maji yalikuwa na joto kali sana kwa kipindi hicho cha zamani watu walipika vyakula vyao hapo, walipika maboga, viazi, kuchemsha mahindi lakini baadaye uharibifu ulipokuwa mkubwa na takataka nyingi zikaletwa.

“Katika eneo hilo maji yalishuka joto kutoka nyuzi joto zilizokuwa zimevuka 100 kurudi mpaka nyuzi joto 45,” anasema.

Anasema mwaka 2019 eneo hilo lilikabidhiwa chini ya TFS na kuanza kulisimamia na kulihifadhi.

“Na tangu uhifadhi umeanza kufanyika katika eneo hilo, nyuzi joto za maji zimerudi tena kwa kiwango cha juu mpaka nyuzi joto 98,” anasema Baragaza.

Anasema maji hayo yana faida nyingi katika mwili wa binadamu kwa ndani ya mwili na nje ya mwili kutokana na madini ambayo yanapatikana kwenye hayo maji.

“Yana mchanganyiko wa madini ya aina tatu ambayo ni calcium, chlorine na sulphur. Haya maji ukiyaoga yanasaidia kuondoa maradhi ya ngozi kama ni mtu mwenye mba, ukurutu, fangasi, maji yanakusaidia.

“Pia kwa kuyatumia ndani ya mwili yanasaidia kuondoa kukaza kwa misuli kwa hiyo watu wanaofanya mazoezi maji haya kulingana na madini ambayo yapo humu yamesaidia tatizo lile la kukaza kwa misuli,” anasema Baragaza.

Anazungumzia pia matumizi ya kiutamaduni katika eneo hilo kuwa maji hayo yanaaminika yanasaidia kuondoa mikosi kwa jamii inayoishi huko ambapo wameamini hivyo tangu ilipokuwa mwanzo mpaka leo hii,” anasema.

Kuhusu watalii katika eneo hilo anasema asilimia kubwa ni wa ndani ya nchi wanaoangalia jinsi mazingira yanavyohifadhiwa.

Naye Mhifadhi Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kutoka TFS, Francis Kiondo, anasema siku ya upandaji miti iliyofanyika Aprili Mosi, mwaka huu katika wilaya hiyo waliadhimisha katika eneo hilo la hifadhi ya chemchemi majimoto.

Anasema eneo hilo ni moja ya maeneo yenye chanzo cha maji yanapotoka kwenye chemchemi yanatiririka hadi kwenye ziwa linalotokana na maji hayo.

Kiondo anasema wanapanda miti eneo hilo kwa kuwa kabla ya TFS kulichukua na kulihifadhi lilikuwa limeharibiwa.

Anasema katika maadhimisho hayo TFS wamepanda miche 1,000 ya matunda ya zambarau na miche ya mikongo ambayo ni miche ya mbao pamoja na miti mingine iliyopandwa.

Anasema TFS katika eneo hilo wanafanya uhifadhi kwa kushirikiana na wananchi.

“Katika eneo hili tunafanya utalii wa majimoto, uvuvi, majengo ya kale hivyo wanakaribisha wananchi kujionea uhifadhi huo,” anasema.

Anasema maji katika eneo hilo yanatiririka kwa mwaka mzima kwa saa moja lita 5,000 kwa saa 24 zinapatikana lita 120,000 ambazo hazipungui kuanzia Januari hadi Desemba.

Mwananchi wa Kitongoji cha Golani, Maimuna Ngingo anasema miaka ya zamani walioga katika eneo hilo kiholela lakini hivi sasa limekuwa hifadhi hivyo wanashukuru kwani imesaidia kutunza mazingira katika eneo hilo.

Anakiri kuwa maji hayo wanapoyatumia yanaondoa upele na magonjwa mbalimbali ya ngozi.

Naye Maulid Tindwa anakiri kuwa chemchemi hiyo imewanufaisha wenyeji wa huko kwani wanayatumia maji yake kwa ajili ya kunywa, kuoga pamoja na kutibu maradhi.

Anawaasa wananchi kutunza mazingira kwa kuacha kukata miti ovyo katika eneo hilo.

Anamuomba Waziri mwenye dhamana kutunza kituo hicho kwani kimesahaulika ili kuvutia watalii wengi wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Katibu Uenezi wa CCM, Bashir Kibopo anasema kuwa hifadhi hiyo ilikuwa inapotea lakini sasa wanashukuru TFS kwa kuitunza.

Anasema wakala huo ulitoa elimu kwa wananchi kuhusu eneo hilo na utunzaji wa mazingira nao wakaridhia lihifadhiwe kwa kuwa hali ilikuwa si nzuri kwani maji yalipungua joto lake.

Kibopo anasema hivi sasa watu katika wilaya hiyo hufanya sherehe mbalimbali za harusi na za kuzaliwa katika eneo hilo.

“Kama hujafika majimoto hujafika Rufiji,” anasema Kibopo.

Mhifadhi Mkuu Kiondo anasema Rufiji ni miongoni mwa wilaya tisa za Mkoa wa Pwani iliyojaliwa kuwa na rasilimali nyingi za maliasili kama vile misitu, wanyamapori na samaki.

“Rasilimali hizi zimekuwa na mchango mkubwa kwenye nyanja za kiuchumi na kijamii zinazozunguka rasilimali hizo kwa taifa kwa ujumla,” anasema Kiondo.

Anasema wilaya hiyo ina misitu ya hifadhi 22 yenye eneo la ekari 142,647, kati ya misitu hiyo misitu 10 yenye ukubwa wa ekari 33,534 ni misitu ya hifadhi ya taifa, misitu mitatu ya ukubwa wa ekari 86,264 ni ya halmashauri ya wilaya na misitu tisa ya ukubwa wa ekari 22,647 ni ya serikali ya vijiji.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mtumwa Said Sandal
Mtumwa Said Sandal
1 month ago

Chat to Live Support

MAPINDUZI.PNG
Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x