Serikali kuvipa nguvu viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki

TABORA: SERIKALI imesema itaendelea kuviwezesha viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki ili kuleta tija kwa wananchi na kuongeza thamani ya mazao hayo kukidhi mahitaji makubwa kwa soko la ndani na la kimataifa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji amesema hayo wakati akihiimisha kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani na siku ya utundikaji mizinga kitaifa iliyofanyika Mei 22, mwaka huu katika kiwanja cha kumbukumbu ya vita Mkoa wa Tabora.

Maadhimisho hayo yaliongozwa na kauli mbiu ya ‘Uhifadhi wa Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Taifa Letu’, kaulimbiu inayokwenda sambamba na mipango ya Taifa ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Waziri amesema ujenzi wa kiwanda kimoja  cha kuongeza thamani mazao ya nyuki katika Wilaya ya Kaliua , mkoani humo  ujenzi umekwishaanza na sasa umefikia asilimia 40.

Dk Kijaji amesema kutokana na mkakati huo Sekta ya nyuki nchini imeendelea kukua na kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa uzalishaji wa asali katika nchi za Afrika Mashariki (EAC), ya pili kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na ya 14 duniani.

Amesema kwa mwaka wa 2025 jumla ya tani 1,569.8 za asali ziliuzwa nje ya nchi yetu ikilinganishwa na tani 951 tu zilizouzwa mwaka 2024 na thamani ya asali iliyouzwa nje ya nchi imeongezeka kutoka Sh  bilioni 11.4 mwaka 2024 hadi kufikia Sh bilioni 19.2 hadi Machi  mwaka 2025.

Dk Kijaji amesema Serikali kupitia wizara itaendelea kuviboresha viwanda vya uchakataji mazao ya nyuki  nchini vikiwemo vya Mkoa wa Tabora ili viweze kufanya kazi kikamilifu na vilete tija kuwasaidia wananchi wetu.

Pia amesema Mpango wa Tanzania iliyo bora umelenga kuongeza uzalishaji wa asali kutoka tani 33,700 hadi tani 75,000 kwa mwaka ambao utawezesha kuona vijana 43,500 wanapata ajira sekta ya nyuki kwa kujiajiri.

“Hatua hii nikiashiria kikubwa kuwa sekta hii inaendelea kukua na kunufaisha wananchi wetu hasa wale walioko kwenye maeneo ya ufugaji nyuki tukiongozwa na mkoa wa Tabora,”amesema Dk Kijaji.

Dk Kijaji amesema sekta ya nyuki inachangia uhifadhi na pato la taifa kuanzia kwenye kaya na ikikadiriwa kuajiri takribani watu milioni mbili.

Waziri pia amempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ni muhifadhi namba moja kwa jitihada zake za makusudi zilizowezesha kuendelea kuimarika na kukua kwa sekta ya ufugaji nyuki hapa nchini.

Waziri pia amehimiza kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ambazo zimekuwa na mchangi mkubwa katika maendeeleo ya taifa na kuchochea upatikanaji wa ajira .

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paulo Chacha, amewapongeza wafugaji wa nyuki wa mkoa huo licha ya kuzalisha asali pia wanasaidia kazi za kiulinzi kwa kuchichua maeneo  misitu inayovamiwa.

Mbali na hayo amesema bado katazo ya kukata miti kwa ajili ya kuzalisha mkaa mkoa humo linaendelea mpaka pale itakapodhihirika ya maeneo ya ukataji ya mkaa au uchomaji mkaa hayatatakuwa hatarishi.

Hivyo amesema Serikali ya mkoa na wizara zindelee kusimama imara ili misitu na mapori yaliyohifadhiwa yasiweze kutoweka kwa dhana ya kuruhusu kukata mkaa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button