Chemical atimiza ndoto sasa ni Dk Lubao

MSANII wa muziki wa hip-hop kutoka Tanzania, Claudia Lubao ‘Chemical’, ameweka historia mpya kwa kufaulu mtihani wake wa mwisho wa shahada ya uzamivu (PhD) na sasa anaitwa rasmi Dk Lubao.
Chemical amehitimu shahada hiyo katika Chuo Kikuu cha St Andrew, Uingereza.
Kabla ya kwenda huko kwa ufadhili wa kimasomo alifanya vizuri pia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikosoma shahada ya kwanza ya sanaa za maonesho, baadaye shahada ya uzamili katika usimamizi wa urithi wa kitamaduni.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Chemical ametoa ujumbe wa shukrani uliogusa wengi akisema: “Nilikuwa na ndoto, na leo nimeamka kama Dk Lubao!”
Ametoa pongezi kwa wasimamizi, idara mbalimbali, jopo la watahini, marafiki, na mashabiki waliompa moyo katika safari hiyo ya kitaaluma.
Chemical, ambaye amekuwa akitamba na nyimbo zenye ujumbe mzito wa kijamii, amethibitisha kuwa mtu anaweza kuwa msanii na bado akang’ara kwenye elimu ya juu.
Shahada yake ya uzamivu inahusiana na urithi wa kitamaduni na mchango wa muziki wa kizazi kipya katika kuwasilisha masuala ya kijamii kama mabadiliko ya tabianchi.
Hiyo ni hatua ya kipekee si tu kwa safari yake binafsi, bali pia kwa wasanii wengine wanaotamani kuunganisha sanaa na taaluma.
Kwa sasa, mashabiki wake wanampongeza kwa mafanikio hayo huku wakisubiri kwa hamu kazi zake mpya zenye ladha ya utafiti na uelewa wa kina.