China, Urusi waongoza mitambo ya nyuklia

BEIJING : MATAIFA ya China na Urusi yameibuka vinara wa maendeleo ya teknolojia ya nyuklia duniani, baada ya kubainika kuwa mitambo yote mipya ya nyuklia iliyojengwa duniani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imetegemea miundo yao.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), kati ya mwaka 2020 hadi 2024, mitambo 38 ya nyuklia iliyoanza kujengwa duniani kote ilitegemea teknolojia ya China au Urusi. Kati ya hiyo, 23 ilifuata muundo wa China na 15 ya Urusi.
Mwaka 2024 pekee, ujenzi wa mitambo mipya ya nyuklia uliongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, ambapo mitambo tisa ilianza kujengwa na inatarajiwa kuongeza megawati 11,000 za umeme ikikamilika.
China iliongoza kwa kuanzisha miradi sita, huku Pakistan ikizindua mtambo wa kwanza wa kizazi cha tatu wa teknolojia ya China nje ya nchi hiyo, na kufikisha jumla ya miradi saba iliyotegemea muundo wa China. Urusi na Misri kila moja ilianza ujenzi wa mtambo mmoja wa nyuklia, yote ikiwa chini ya usanifu wa Urusi.
Katika miaka iliyotangulia, mwaka 2023 uliona uanzishaji wa mitambo sita—mitano ya China na mmoja wa Urusi; mwaka 2022 miradi minane ilizinduliwa (mitano ya Urusi, mitatu ya China); mwaka 2021 miradi 10 (sita ya Urusi, minne ya China); na mwaka 2020 miradi mitano (minne ya China, mmoja wa Urusi).
Hadi Februari 2025, jumla ya mitambo 62 ya nyuklia ilikuwa inajengwa katika nchi 15 duniani, ikiwa na uwezo wa pamoja wa kuzalisha karibu megawati 70,000.SOMA: China, Urusi kuendeleza uhusiano wa nyuklia
China inaongoza kwa kuchangia karibu nusu ya uwezo huo, ikithibitisha kuimarika kwa nafasi yake kwenye soko la nyuklia duniani. Kiasi cha megawati 33,000 kati ya hizo kinatoka kwenye miradi yake.
Nchi kama Misri, India na Uturuki kila moja inajenga mitambo yenye uwezo wa takriban megawati 5,000, huku Japan, Korea Kusini, Uingereza na Slovakia zikiwa na jumla ya megawati 9,500 katika ujenzi.
Kwa mwaka 2024 pekee, uwezo wa nyuklia duniani uliongezeka kwa zaidi ya megawati 7,000, na kufikisha jumla ya megawati 420,000 za uzalishaji.Ongezeko hilo limechangiwa na kukamilika kwa miradi sita mikubwa ya nyuklia—miwili nchini China, na mingine nchini Ufaransa, India, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Marekani.