China yafungua milango zaidi kwa Tanzania
ziara ya Chongolo, wajumbe yazaa matunda

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema ziara ya viongozi wake nchini China imezaa matunda kwa kuwa wawekezaji wengi wa taifa hilo watakuja kuwekeza nchini.
Hayo yamesemwa leo Aprili 28 jijini Dar es Salaam na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Sophia Mjema ambaye amesema wawekezaji hao wa China watawekeza katika sekta ya elimu stadi, kilimo, afya na kubadilishana uzoefu namna China walivyoweza kuondoa umaskini na kuinua uchumi wao.
Amesema kuwa China imeweza kufanikiwa kupitia majimbo matatu na kwamba kama Tanzania ina nafasi ya kufanya mapinduzi ya kimaendeleo sambamba na kuondoa umasikini.
“Rais Samia Suluhu Hassan amefugnua milango ya mahusiano na ushirikiano kimataifa kwani ziara hii imekuwa na mafanikio makubwa ambayo yatakuwa chachu ya kuendelea kuchagiza na kudumisha uhusiano katika nyanja mbalimbali kwa maslahi ya vyama vyetu na wananchi wa nchi zetu mbili.”Amesema Mjema.
Ziara hiyo ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na wajumbe 20 wa Halmashauri Kuu na wataalamu wawili wa chama hicho, ni utekelezaji wa makubaliano na maelekezo yaliyotolewa na viongozi wakuu, ikiwemo Rais Samia na Katibu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jingping.
Mjema amesema viongozi hao walikubaliana kupandisha hadhi ya uhusiano kati ya CCM na CPC kati ya Tanzania na China kwa kuwa na uhusiano maalumu wa kimkakati katika nyaja za elimu na ufundi stadi, habari na mawasiliano, kilimo, uvuvi, afya na viwanda.
Amesema kupitia ziara hiyo wamejifunza na na kuona jinsi wenzao walivyoweza kufungua nchi kiuchumi kupitia majimbo ya Shengzen, Guandong na Guanzhou.
‘’Aprili 17 hadi 28, mwaka huu, Chongolo na ujumbe wake walitembelea majimbo matatu nchini China ambayo Shengzen, Guandong na Guanzhou katika ziara hiyo.
Pia, walikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa CPC Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambao ni, Mkurugenzi wa Kamisheni ya Mambo ya Nje wa Kamati Kuu ya chama hicho, Wang Yi, Waziri wa Idara wa Mambo ya Nje ,Liu Jianchao, wengine ni Naibu Waziri wa Idara ya Mambo nje, Li Mingxiang , Katibu wa chama hicho jimbo la Hebei, Ni Yuefeng na Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya CPC jimbo la Guandong, Wang Ruijun.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata alisema walichojifunza China ni jinsi nchi hiyo ilivyowawezesha vijana kufanya kazi na kujiajiri maeneo mbalimbali.