Chongolo amuita Waziri wa Maji Lupeta

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amemtaka Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwenda Mpwapwa kabla yeye hajamaliza ziara yake ili kujibu wananchi kuhusu miradi ya maji ambayo haijakamilika kwa wakati ukiwemo mradi wa maji wa Kijiji cha Lupeta.

Chongolo amesema hayo wilayani hapo jana   Juni 15,2023 wakati alipotembelea katika kijiji hicho ikiwa ni ziara yake ya kutembelea majimbo yote ya Mkoa wa Dodoma,kukagua miradi ya maendeleo ya Mkoa wa Dodoma.

Amesema,  Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh bilioni 2 kwajili ya mradi wa maji katika kijiji hicho lakini Mkandarasi anahitaji kulipwa Sh milioni 600 iliakamilishe.

“Hapa nimeona Mkandarasi anahitaji milioni 600 na kidogo kabla sijaondoka mkoa huu Waziri wa maji atakuja hapa, Ili tujue hizo fedha anakuja nazo au analeta lini?”

“Mimi kabla sijaondoka hapa atakuja Waziri na mimi naondoka hapa tarehe 25 na akija hapa aseme mradi unakamilika lini na fedha inakuja lini,hatuwezi kukaa tunasema maneno mengi tunataka matokeo,”amesema Chongolo.

Akijibu maombi ya wananchi kwa chama kuhusu kujengewa Zahanati katika Kijiji cha Lupeta na Bumika Chongolo amesema atafanyia kazi changamoto hiyo.

Aidha katika kuunga mkono juhudi za wananchi, Chongolo amechangia mifuko 50 ya saruji kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji Cha Makutupa huku akiagiza hadi kufikia Septemba mwaka huu zahanati hiyo ikamilike na kuanza kufanya kazi.

Pia, Chongolo ametumia fursa hiyo kuwahimiza Wazazi na walezi kupeleka Watoto mashuleni huku akisistiza kuwa Rais ametoa fedha kwajili ya ujenzi wa chuo cha veta hivyo wakasome

“Niwaambie, Elimu sio bure bali ni bila malipo yoyote kutoka kwa wazazi yupo mtu ambaye kaamua kuubeba mzigo wa kulipia ambapo ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye anayeoongoza Serikali ya awamu ya sita hivyo Wazazi mnatakiwa kumlipa ukarimu wake kwa kuwapeleka watoto shuleni wakapate haki yao ya kupewa Elimu,”amesema Chongolo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button