KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),amekasirishwa na kutelekezwa kwa kituo cha Afya Mikese,mkoani Morogoro kilichokamilika zaidi ya miaka mitatu sasa lakini hakitumiki kutoa huduma kwa wananchi.
Hivyo amempa siku 14, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),Angela Kairuki kufika kituoni hapo kujionea hali halisi.
Chongolo amesema hayo leo mara baada ya kukagua kituo hicho,akiwa katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Morogoro, kuangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo,uhai wa chama na kuzungumza na wananchi.
Akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa kituo hicho, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Mikese,Piencia Mushi amesema ujenzi huo ulianza mwaka 2019 baada ya kubomolewa kwa Zanahati ya Kijiji ili kupisha ujenzi wa Reli za Kisasa ya (SGR).
Amesema ujenzi ulianza kufanywa na Kampuni ya Yapi Merkez iliyotakiwa kulipa fidia ya zahanati iliyobomolewa kupisha ujenzi wa reli hiyo na gharama za jengo ulikuwa Sh milioni 105 na vifaa tiba gharama zilikuwa Sh milioni 200.
Aidha awamu ya pili ujenzi wa majengo kama chumba cha upasuaji,nyumba ya mtumishi,maabara,chumba cha kuhifadhi maiti na jengo la mama na mtoto umegharimu shilingi milioni 400 na halmashauri ikaongezea sh milioni 60.5
Hata hivyo pamoja na hayo yote bado kituo hicho hakitumiki na huduma zinazotolewa ni zile za kiwango cha zanahati.
Akizungumzia hilo,Chongolo alikerwa na hali hiyo na kusema serikali imepeleka fedha ili wananchi wake wapate huduma lakini baadhi ya watendaji hawatimizi wajibu wao hali inayofanya pia baadhi ya watu waanze kumsimanga Rais Samia Suluhu Hassan.
“Watu wetu hapa wanakaa kienyeji hawatimizi wajibu wao,nitawasiliana na Waziri wa Tamisemi na ndani ya siku 14,aje hapa ajionee,vifaa vipo vimekaa tu wakati huduma zinatakiwa zitolewe,”amesema Chongolo.