Chris alivyoandika rekodi ya kuwa bilionare kwa dk 2 tu

U.S.A, Pennsylvania: Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Chris Reynolds ameandika rekodi ya kuwa binadamu wa kwanza kuwa quadrilionea na mtu aliyewahi kuwa na utajiri mkubwa zaidi kwa muda mfupi zaidi wa dakika 2.

Ilikuwaje, Iko hivi; Chris kutoka Pennsylvania alijaribu kuangalia akaunti yake ya PayPal ambayo aliifungua mwaka 2013 na alitarajia kukuta dola 140 ambayo alikuwa amehifadhi huko. Kwa mshtuko alikuta akaunti yake ikiwa na kiasi cha dola za Marekani quadrilioni 92. Idadi kamili kwa tarakimu ilisoma $92,233,720,368,547,800.

Mwanzoni, Chris alikuwa na wasiwasi kuwa pengine anadaiwa na mtu matrilioni ya dola. Akaamua kuchapisha taarifa hiyo kwenye ukurasa wake wa Facebook ili kupata ufafanuzi, hata hivyo, haikuchukua muda akahakikishiwa kuwa takwimu hizo ni ‘amana’ na sio ‘deni.’

Kwa Chris kiasi kikubwa cha pesa alichowahi kukiona kwenye akaunti yake kilikuwa ‘dola 1,000 na zaidi’ ambazo alipata baada ya kuuza matairi ya zamani ya BMW kwenye mtandao wa eBay.

Mtandao wa UniLad umeripoti kuwa, Chris aligundua kuwa kuna hitilafu kwenye mfumo wa PayPal hivyo akajiondoa na kurudi tena ndipo alipokuta akaunti ikiwa haina hata centi.

Pesa zilikuwa zimeondoka. Hata hivyo amesema alikuwa tayari ameshajua nini cha kufanya. Moja ikiwa ni kulipa deni lote la taifa, aliliambia gazeti la Philadelphia Daily News. Pia alipanga kununua timu ya baseball ya Philadelphia Phillies. Timu hiyo inatajwa kuwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 2.58 kiasi ambacho ilikuwa ni ‘chenji ya mboga’ kwa ‘utajiri’ wake wa muda mfupi.

PayPal ilisema katika taarifa: ‘Hili ni kosa na tunashukuru kwamba Bw. Reynolds alielewa kuwa ndivyo ilivyokuwa.’

Kampuni hiyo pia ilijitolea kutoa kiasi cha pesa ambacho hakijatajwa kwa shirika la hisani lililochaguliwa na Chris.

Kwa bahati nzuri, Chris alipata ucheshi katika jaribu hilo, akisema lingeweza kutokea kwa sababu ‘kuna mtu alikuwa akiburudika.’

PayPal iliongeza katika taarifa ‘Tunafikiri inatia moyo kwamba aliamua kutumia tukio hili kutoa mchango kwa sababu anayoamini.

‘Na tunatumai kuheshimu roho hii kwa kuchangia jambo analochagua – tumemfikia ili kutoa ofa hii na kumjulisha kuwa tunashukuru kwamba yeye ni mteja!’

 

Habari Zifananazo

Back to top button