Chui bingwa Kombe la KNK 2024 Bukombe

MASHINDANO ya Kombe la KNK 2024 yaliyoandaliwa na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati , Dk Doto Biteko yamehitishwa kwa kishindo huku timu ya Chui kutoka Kata ya Butinzya ikiibuka kidedea dhidi ya timu Nyuki ya Kata ya Bugerenga mkoani Geita.

Mashindano hayo yaliyohusisha timu 246 kutoka kata 17 za Wilaya ya Bukombe yamehitimishwa kwenye uwanja wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe – Kilimahewa Mkoani Geita na kushuhudiwa na mamia ya wananchi na viongozi ambapo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alikuwa mgeni rasmi.

Advertisement

 

Dk. Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe amesema mshindi wa ligi ya KNK ya Bukombe na mshindi wa ligi ya Bashungwa Karagwe watakuwa na mechi ya kirafiki ambayo itawaunganisha vijana na kukuza vipaji.

SOMA: Dk Biteko awapa somo wasanii

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za za Mitaa kwa kuchagua viongozi bora na wenye uwezo wa kuwahudumia Wananchi.

Kwa upande wake Waziri Bashungwa amempongeza Dk Biteko kuendelea kuunga mkono kwa kasi jitihada za Rais, Dk Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya michezo nchini kupitia ligi ambayo inaibua na kukuza vipaji na kuimarisha afya.

“Naibu Waziri Mkuu nikupongeze kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya, hii ni mara ya pili unanipa heshima hii, nilipokuja hapa mwaka 2021 ligi ilikuwa imefana lakini hii ya mwaka 2024 hakika imeboreshwa kwa kiwango kikubwa”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameahidi kutoa shs milioni 15 kuboresha Uwanja wa Kilimahewa wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ambao unatarajiwa kuwekwa nyasi na kusaidia kuongeza mapato ya Halmshauri.

Kuhusu suala la miundombinu ya barabara, Bashungwa amemuhakikishia Naibu Waziri Mkuu kuwa, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS), tayari imeanza manunuzi ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ushirombo – Katoro (km 59) kwa kiwango cha lami na kusisitiza hadi kufika mwishoni mwa mwezi Disemba 2024 kazi za ujenzi zitakuwa zimeanza.