Confucius, JUYE wadhamini 27 kusoma Kichina

DAR ES SALAAM: WANAFUNZI 27 wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamepata udhamini wa kuendelea na masomo ya lugha ya Kichina, baada ya kuonyesha umahiri katika ngazi mbalimbali za mafunzo hayo. Udhamini huo unahusisha kulipiwa ada za masomo kama sehemu ya kutambua juhudi na bidii walizozionyesha wanafunzi hao.
Hafla ya utoaji wa udhamini huo imeandaliwa na Kampuni ya Saruji ya JUYE Tanzania Ltd kwa kushirikiana na Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa taasisi husika pamoja na wanafunzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtanzania wa Taasisi ya Confucius, Dk Mussa Hans amesema udhamini huo utawasaidia wanafunzi wenye uwezo na wasio na uwezo kuendelea na hatua zinazofuata bila kukwama, pia ameishukuru JUYE kwa kuendelea kuunga mkono na kutoa motisha kwa wanafunzi hao.

Dk. Hans ameeleza kuwa mfumo wa udhamini huo umezingatia viwango vya ufaulu wa wanafunzi, ambapo waliopita vizuri katika hatua ya kwanza wamelipiwa ada ya kusoma hatua ya pili, na waliopita vizuri katika hatua ya pili wamelipiwa ada ya kusoma hatua ya tatu. Wanafunzi waliopata matokeo mazuri katika hatua ya nne wamepewa fedha taslimu kama zawadi.
Ameafanua kuwa kiwango cha udhamini kinatofautiana, ambapo baadhi ya wanafunzi wamepata ufadhili wa asilimia 100, wengine asilimia 90, asilimia 70, na wengine asilimia 50. Alisema ufadhili wa asilimia 50 umetolewa kama motisha, kwani idadi ya wanafunzi waliostahili ni kubwa.
SOMA ZAIDI: China yafungua daraja kubwa duniani
Kwa mujibu wa Dk. Hans, lengo la utaratibu huo ni kuwahamasisha vijana kusoma kwa bidii wakijua kuwa wana nafasi ya kupata ufadhili, jambo litakalowasaidia pia kutambulika katika taasisi nyingine za Confucius.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni ya JUYE Tanzania Ltd, Bi. Xu Hongjuan, amesema tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Confucius mwaka 2013, imekuwa daraja muhimu la kubadilishana elimu na tamaduni kati ya China na Tanzania. Aliongeza kuwa zaidi ya wanafunzi 60,000 wamenufaika na ushirikiano huo kati ya mataifa hayo mawili.

Bi. Xu alisema ujuzi wa lugha ya Kichina unaotolewa kupitia taasisi hiyo unawasaidia vijana katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uchumi, biashara, mabadilishano ya kitamaduni na misaada ya kielimu. Aidha, alisema lugha hiyo imekuwa mhimili muhimu katika kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya China na Tanzania.
Alimalizia kwa kusema kuwa, mbali na shughuli za kibiashara, Kampuni ya JUYE Tanzania Ltd imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Naye Imran Khatau, mmoja wa wanafunzi walionufaika na udhamini huo, alisema lugha ya Kichina si ngumu kama inavyodhaniwa na kwamba aliamua kuisoma kutokana na fursa nyingi zinazopatikana kupitia lugha hiyo.
“Nilishauriwa na watu wawili kuwa kwa sasa kuna makampuni mengi ya Kichina nchini, hivyo ni muhimu kujifunza lugha yao ili kurahisisha shughuli za biashara. Nilikuja nikiwa naamini Kichina ni lugha ngumu, lakini baada ya kuanza kujifunza nimegundua kuwa ni rahisi,” amesema Imran.




