CRDB yarekodi faida Sh bil 206 robo ya kwanza

DAR ES SALAAM; CRDB Bank Plc imeendelea kuthibitisha ubora wake katika sekta ya benki baada ya kuongoza kwa faida katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, ikirekodi faida ya Shilingi bilioni 206 baada ya kodi sawa na ongezeko la asilimia 18.9.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela, amesema kuwa ongezeko la faida linaakisi utekelezaji mzuri wa mkakati wa biashara wa benki hiyo, uliolenga kuimarisha ushindani na ufanisi wa huduma.
Amesema matokeo hayo yanaonesha ukuaji thabiti wa benki hiyo, ambayo sasa inaongoza katika viashiria vikuu vya kifedha na kiutendaji.
Amesema mizania ya benki imeimarika zaidi, ambapo jumla ya mali imeongezeka kwa asilimia 7.1 na kufikia Shilingi trilioni 23.9.
“Aidha mikopo kwa wateja imekua kwa asilimia 6.8 hadi Sh trilioni 14.7, huku amana za wateja zikiongezeka kwa asilimia 9 na kufikia Sh trilioni 16.3,” amesema.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na dhamira ya benki kutoa thamani bora kwa wateja wake, kuchochea ukuaji wa uchumi katika masoko inayohudumia, pamoja na kuendelea kujenga thamani endelevu kwa wanahisa wake.



