CRDB yawatangazia raha wakulima Mtwara

BENKI ya CRDB Kanda ya Kusini, imewashauri wakulima wa zao la korosho mkoa wa Mtwara kutumia tembo card, wakati wa kufanya malipo mbalimbali katika benki hiyo kwani ina faida nyingi.

Pia imesema wakulima pamoja na wananchi wengine watakaotumia tembo card, wataweza kujishindia nafasi ya kwenda Qatar kushiriki michuano ya Kombe la Dunia.

Meneja Usimamizi wa Mali na Huduma za Benki CRDB Kanda ya Kusini, Leavan Maro alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Tisha na Tembo Card, ambayo imeandaliwa kwa ajili ya wateja wa benki hiyo.

“Kampeni hii (Tisha na Tembo Card), imeandaliwa mahususi kwa ajili ya wateja wetu kuweza kushiriki na kupata zawadi ambazo benki imeziandaa kwa makundi tofauti tofauti,” amesema.

Maro amesema benki hiyo itatoa takribani shilingi milioni tatu kwa mwezi, kwa wateja ambao wataweza kushiriki kwa wingi kwa kutumia kadi zao (Tembo Card), kwa matumizi mbalimbali.

“Niwasihi sana wateja wa Kanda ya Kusini kushiriki kwa wingi, kwa sababu naamini kabisa Kanda ya Kusini ni Kanda ya ukomavu katika suala la biashara, hivyo tutatamani sana kuwaona wateja wa Kanda ya Kusini wakishinda kwenda Qatar na kushiriki kwenye zawadi nyingine nyingi,” amesema. Kampeni itaendeshwa ndani ya miezi 3.

 

Habari Zifananazo

Back to top button