DAKTARI Bingwa wa Moyo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Pedro Pallangyo amesema inashauriwa mtu kula chakula cha jioni saa tatu hadi nne kabla ya kulala ili kukabiliana na ongezeko la mafuta mwilini.
Akizungumza na Dailynews Digital katika mahojiano maalum ,Dk Pedro amesema mtu akila,chakula na kulala baada ya muda mfupi chakula kinakuwa hakijameng’enywa hivyo mafuta kuwa mengi hali itakayoongeza uzito mwilini.
“Kuna changamoto ya ulaji hasa wakati wa jioni na wataalamu wanashauri kula saa tatu hadi nne kabla ya kulala kwani uzito unapoongezeka mtu anakuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza.
Amesema sababu zingine hatarishi zinatokana na mtindo wa maisha ambao unasababisha uzito mkubwa kupindukia ,tabiabwete,msongo wa mawazo,ulaji usiofaa hasa wa chumvi na mafuta ,matumizi ya tumbaku na matumizi makubwa ya pombe .
Amefafanua kuwa matumizi ya pombe, tumbaku na ulaji usiofaa hayaleti athari kwa muda mfupi bali inachukua muda mrefu .
“Na kila pombe ina kiwango cha kilevi ambacho kimeshauriwa kisizidishwe kwa kuangalia viwango mfano kwa pombe kali kunywa shoti moja au mbili kwa siku ,mvinyo kwa mwanamke glasi mbili na mwanaume tatu na kwa bia chupa moja au mbili kwa wanawake na mbili hadi tatu kwa wanaume.
Aidha amebainisha kuwa mama mjamzito haruhusiwi kunywa pombe wala kutumia tumbaku hata kidogo kwani mtoto katika hatua za ukuaji zinaweza kumuathiri.
“Kuna sababu zingine kama umri unavyozidi kuwa mkubwa hatari ya mtu kupata magonjwa ya moyo inaongezeka pili ni jinsia kuna mgonjwa ambayo yanaweza zaidi kuvamia jinsi ya kike na mengine kiume.
Ameongeza “Tatu ni kuwa na historia Chanya kutoka katika familia ya magonjwa ya moyo ,mtu anayetoka kwenye familia ambayo watu wanashinikizo la damu au kisukari wanahatari zaidi kupata magonjwa.
Amesema hakuna dalili za awali kwa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu hadi pale tatizo linapojitokeza
Ameeleza kuwa dalili zisizo za moja kwa moja ni kuumwa kichwa,moyo kwenda kasi,kupumua kwa shida,ganzi na maumivu kwenye moyo.
“Tulifanya tafiti tuligundia asilimia 25 hadi 35 wanashinikizo la damu katika jamii na tumeenda mikoa 15 kwaajili ya tiba mkoba hadi sasa JKCI inamachapisho 70 ya tafiti mbalimbali.
Dk Pallangyo ameshauri watu kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka ili wakigundulika na tatizo wapate matibabu haraka.