Dar, Pwani vinara kusajili miradi ya uwekezaji
MKOA wa Dar es Salaam umeongoza kwa kusajili idadi kubwa ya miradi ya uwekezaji katika kipindi cha Januari na Desemba 2024.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amebainisha hayo jana Dar ea Salaam katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari kueleza mafanikio ya ukuzaji na maboresho ya mazingira ya biashara 2024 na mwelekeo wa 2025.
Profesa Kitila alisema miradi ya uwekezaji 356 kati ya 901 ambayo ilisajiliwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, ilisajiliwa katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Alitaja mikoa mingine iliyofuatia kwa idadi kubwa ya kusajili miradi ya uwekezaji katika kipindi hicho ni Pwani iliyosajili miradi 166, Arusha 64 na Dodoma 47 sawa na asilimia 70.3 ya miradi yote iliyosajiliwa.
“Hii niliyoitaja iko juu, lakini miradi imesajiliwa katika kila mikoa,” aliongeza Profesa Kitila alitaja mikoa ambayo haifanyi vizuri katika kusajili miradi kuwa ni Tabora, Rukwa, Songwe, Singida na Kagera.
“Mikoa ambayo iko chini kidogo ni Mkoa wa Tabora ulisajili mradi mmoja tu, Rukwa minne, Singida sita, Songwe mitano, Kagera mitano, Iringa 11, Manyara tisa na Mara nane. Mtwara ilisajili 12, Mbeya 20, Kigoma 18 na Geita 18,” alibainisha.
Aidha, alisema serikali inaangalia namna bora ya kupunguza utitiri wa kodi na tozo katika biashara nchini ili wawekezaji na wafanyabiashara wafanye biashara bila bughudha na kufaidika na biashara zao.
“Lazima nikiri hapa kwa niaba ya serikali bado tuna changamoto na ni kitu cha kukifanyia kazi katika mpango mpya wa mazingira bora… Nimetoka Manyara juzi mfanyabiashara mmoja aliniambia kwa siku anaweza kutembelewa na taasisi za serikali tisa kumkagua, hii haikubaliki na tunataka tupunguze hili kwa sababu ni moja ya njia za haraka kuua biashara,’’ alieleza Profesa Kitila.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri alisema wamerahisisha taratibu za kusajili miradi kwa wawekezaji ambako mwekezaji atasajili mradi wake ndani ya saa 24 baada ya kukamilisha taratibu na vigezo vyote.
“Mwekezaji yeyote akikamilisha vigezo vya kusajiliwa kuwa mwekezaji na TIC kwamba ana mtaji, eneo lake la biashara ana hati na mpango wa biashara, usajili wa Brela na TRA atapata cheti cha uwekezaji ndani ya saa 24,” alisema Teri.
Aidha, Teri aliitaja baadhi ya miradi mikubwa ya uwekezaji iliyosajiliwa 2024 katika Mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni Mradi wa Hoteli ya Southern Sun ambao umegharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni mbili, Kunduchi Mall zaidi ya Dola milioni 20 na biashara na makazi miradi 11 ya zaidi ya Dola milioni nne.
Mingine ni Mradi wa samani wa wawekezaji wa Kituruki wa Dola za Marekani milioni sita, mradi wa umemejua wa Kampuni ya Saruji ya Wazo wa Dola milioni tisa, mradi wa kiwanda cha tumbaku Dola milioni sita na mradi wa Kampuni ya DP World ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambao ni Dola milioni 250 na uliotoa ajira 253.



