Dar: Wiki ya afya na ustawi yazinduliwa

DAR-ES-SALAAM : TAASISI ya Bloom Wellness Tanzania imezindua Wiki ya Afya na Ustawi Tanzania, itakayofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuhamasisha uelewa wa kitaifa kuhusu afya ya mwili na akili kwa njia jumuishi na endelevu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwanzilishi Mwenza wa Bloom Wellness, Dk Sophia Byanaku, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kujenga jamii inayojali afya kwa misingi ya sayansi ya kisasa sambamba na maadili ya Kitanzania. “Ustawi unapaswa kuwa wa kila mtu, sio tu kwa lishe na mazoezi, bali pia kwa kujijali, kujijenga kiakili na kuungana kama jamii,” alisema.
Dk Byanaku alifafanua kuwa Wiki ya Afya na Ustawi itakuwa jukwaa la kila mwaka la kukuza majadiliano, kuleta msukumo wa mabadiliko na kuongeza hamasa ya kutekeleza afya bora katika maisha ya kila siku.
Aidha aliongezea kuwa tukio hilo litajumuisha vipengele mbalimbali vikiwemo warsha za afya, mihadhara ya kitaalamu, vipindi vya mazoezi ya mwili, darasa za kutafakari, maonesho ya mapishi ya lishe bora, na kampeni za uhamasishaji kuhusu afya ya akili.
SOMA: Wenye afya ya akili wapelekwe vituo vya afya
Mtaalamu wa Mawasiliano ya Afya kutoka Wizara ya Afya, Grace Msemwa, alitoa wito kwa wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika wiki hiyo. “Tunaunga mkono kikamilifu juhudi hizi na tunatarajia ushirikiano wa muda mrefu na Bloom Wellness katika kukuza afya ya jamii,” alisema Msemwa.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Afya Kazini, Baldwina Olirk, alisisitiza umuhimu wa kula mlo kamili kwa mpangilio sahihi, akionya dhidi ya ulaji wa vyakula vya haraka. Alisema ulaji huo huongeza hatari ya kupata magonjwa kama vile unene uliopitiliza, shinikizo la damu na kisukari, akisisitiza kuwa lishe bora ni nguzo ya msingi ya ustawi wa afya.