Daraja la Mpiji lafunguliwa upande mmoja

DAR ES SALAAM: HATIMAYE daraja la Mto Mpiji ambalo ni mpaka wa Bagamoyo Pwani na Dar es Salaam lililokuwa limefungwa kwa muda ili kupisha ujenzi baada ya kuwa hatarini kukatika kutokana na mvua zinazonyesha limefunguliwa upande mmoja kuruhusu magari kupita.

Jana usiku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amekesha katika eneo hilo akiwepo na watendaji wengine wa serikali na wakandarasi ili kuhakikisha ujenzi unaendelea ili kuruhusu barabara hiyo kuendelea kutumika.

Jitihada hizo zimezaa matunda kwa kuwa tayari walau upande mmoja magari yameruhusiwa kupita huku ujenzi ukiendelea. Akiwa katika eneo la tukio ambayo ni barabara ya Bagamoyo, Chalamila alisema,

“Tumekutana katika daraja la mto Mpiji kutokana na hitilafu iliyotokea ya kukatika kidogo kwa daraja, hivyo tupo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Sadi Mtambule pamoja na mainjinia wakuu wa Tanroads katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

“Nawapa pole kwa wale wote ambao wanatumia sana daraja hili lakini pole hii iambatane na tahadhari tuliyoitoa kwamba tuendelee kuchukua tahadhari kwa mvua nyingi ambazo zinaendelea kunyesha.

“Jambo ambalo limetokea hapa ni hitilafu ya daraja ambalo tumewahi kwa maana kwamba kusitokee na maafa ya aina yoyote na kwa maana hiyo kwa sasa tumefunga kwanza upitikaji wa daraja hili na hasa kwa magari ili tuweze kupata majawabu ya haraka mpaka inapofikia asubuhi tuwe tumeshapata majibu ya kutosha,” alisema.

Amesema kwa mantiki hiyo kwa wale ambao wanaelekea njia za Bagamoyo wametoa njia mbadala, kwa wale ambao wanatoka mjini kwa maana ya upande wa Dar es Salaam wanaelekea Bagamoyo kama bado hawajatoka huko wapitie barabara ya Morogoro lakini kama wamekwisha toka kuna njia mbalimbali.

“Unaweza kupita Massana kwenda Goba lakini pia ukapita Kibaoni kwenda Mbezi Mwisho mpaka kutokea Kibamba, lakini vile vile unaweza ukapita pia Kibaoni kwenda Mbezi kwa Yusuf zote hizo ni njia zinapitika bado pia unaweza ukapita mpaka kuelekea Mabwepande.

“Lakini kwa wale ambao walikuwa wanatoka Bagamoyo kuelekea Dar es Salaam wanaweza kupitia Baobao sekondari wakaenda moja kwa moja mpaka Kidimu, mpaka Kibaha maili moja stendi zote hizi ni njia mbadala,” alisema.

Ameonya tabia za madereva wanaopenda kujaribu kwa magari kwa kuwaeleza barabara hiyo wameifunga kwa muda kwenye daraja hilo.

“Nitoe msisitizo kwamba tusijaribu kina cha maji kwa miguu yetu wenyewe hapa tumefunga lakini mameneja wa Tanroads wa mikoa miwili wanatumia kila akili ambayo wamezaliwa nayo na ile ya taaluma kuhakikisha kuwa kesho asubuhi daraja hili linaanza kupitika,” alisema.

Amesema akiwa na viongozi wenzake atakesha katika daraja hilo mpaka asubuhi ili kuhakikisha daraja linaanza kupitika haraka iwezekanavyo.

Naye Abiud Mkumbo meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania, amesema chanzo cha kuharibika kwa daraja hilo kunasababishwa na maji mengi kutoka maeneo mbalimbali kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Amesema wanasubiri magari yapeleke malighafi za ujenzi katika eneo hilo ili waanze kujenga.

“Kwa usalama maana yake ni kwamba tunataka tufunge mawe ya zege yakija yatawekwa upande huu.Tunataka kuanza ujenzi kwa ajili ya kuokoa maji yalikuwa ni mengi yaliyopita yalijaa mpaka kwenye kofia,” alisema.

Amesema daraja hilo lilishapata tatizo kwenye zile mvua za mwanzo ambazo katikati kwenye nguzo mbili zilikuwa zimeliwa na maji.

Habari Zifananazo

Back to top button