DAS Arusha aonya vikwazo utendaji

ARUSHA: KATIBU Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk.Toba Nguvila amesema hatavumilia vikwazo vya kiutendaji wala urasimu unaokwaza wawekezaji katika sekta ya utalii mkoani humo ikiwemo migogoro kwa wananchi.

Dk Nguvila ametoa kauli hiyo jijini Arusha wakati wa mapokezi yake, mara baada ya kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo, kisha kuzungumza na watumishi wa umma wa mkoa huo waliojitokeza kumpokea.

Amesema Mkoa wa Arusha unapaswa kuimarika zaidi katika sekta ya utalii kwa kuwa kila wilaya ina vivutio vyake, hivyo si busara kwa baadhi ya watendaji kuweka vikwazo na urasimu usio wa lazima unaoweza kudhoofisha sekta hiyo.
“Kila halmashauri iainishe vipaumbele vya sekta ya utalii katika bajeti zake. Uwepo wa vikao vya kimataifa ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi,sina adui wala rafiki wa kudumu, ninachohitaji ni ushirikiano katika utendaji kazi,” amesema.

Amesisitiza kuwa hataki kusikia migogoro isiyo na tija miongoni mwa wakurugenzi, wakuu wa idara na taasisi mbalimbali, badala yake akataka kuwepo kwa upendo, amani na ushirikiano kazini.



