Dawa inatokota wezi miradi ya Serikali

MWANZA: MKUU wa Opereseheni za Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Aloyce Nyantora  amesema Jeshi la Polisi halitosita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watu wanaojihusisha na wizi wa vifaa vya ujenzi katika miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.

Nyantora ametoa onyo hilo wakati akiongoza oparesheni ya doria ya kuhimalisha ulinzi katika Ziwa Victoria ambapo doria hiyo imeendeshwa kwenye  mialo mbalimbali na ilipo miradi ya Serikali akianzia Wilaya ya Ilemela na kumalizia eneo la Kigongo-Busisi ambapo elimu ya usalama kwa abiria waliokuwa wanasafiri kwenye Vivuko vya MV Mwanza na MV Sengerema ilitolewa.

Akiwa katika eneo hilo la Busisi wilayani Sengerema, ulipo mradi wa Daraja la JPM, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa, ACP Ramadhani Sarige ametoa elimu ya usalama kwa abiria na wananchi wa eneo hilo ambapo amewasihi kuvaa maboya wakati wote wakiwa majini na  kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la Polisi ili kuweza kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Baadhi ya wasafiri na wananchi wa maeneo ambayo doria hiyo imepita wamelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kazi hiyo, pia wamehimiza uendelevu wa doria katika Ziwa Victoria huku wakiongeza kuwa wanapoona doria hizo wanakuwa na amani.

Maeneo mengine yaliyofikiwa na doria hiyo ni Mwanza Kusini inapojengwa meli ya Kisasa MV.MWANZA HAPA KAZI, Reli ya Kisasa ya SGR, Mwalo wa Luchelele, Mwasonge, Kisiwa cha Saa Nane na Chuo cha Ualimu Butimba.

Mwishoni mwa mwezi Desemba, 2023 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa alizindua doria hiyo alipotembelea Kisiwa cha Gana Wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya kukagua nyumba iliyotolewa na mkazi wa kisiwa hicho ili itumike kama kituo cha polisi ambapo alisema kuwa  doria hiyo ni endelevu na ina lengo la kutokomeza uhalifu wote mkoani Mwanza.

 

Habari Zifananazo

Back to top button