DC Bariadi atoa maelekezo madeni ya maji

SIMIYU; Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu,  Simon Simalenga ameuagiza uongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani humo kukata huduma ya maji kwenye taasisi zote za serikali, ambazo zinadaiwa bili za maji.

Simalenga ametoa agizo hilo leo, kwenye mkutano mkuu wa pili wa wadau wa maji na vyombo vya utoaji huduma ya maji (CBWSOS), baada ya Kaimu Meneja wa Ruwasa Wilaya, Herry Magoti kuelezea ukubwa wa changamoto hiyo.

Katika taarifa yake Kaimu Meneja huyo wa RUWASA, amesema kuwa taasisi nyingi za serikali zikiwemo shule za msingi, sekondari, pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya ndizo zinaongoza kwa kutolipa bili.

“ Kama Ruwasa wilaya tunayo changamoto kubwa ya taasisi za serikali kama shule za msingi na sekondari na vituo vya kutolea huduma za afya, zimekuwa zikilimbikiza madeni, hazilipi kwa wakati bili za Maji,” amesema Magoti.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ruwasa na msimamizi wa vyombo vya utoaji huduma ya maji, Asha Malimungu amesema kuwa baadhi ya shule na vituo vya kutolea huduma za afya wanadaiwa bili ya hadi miezi sita.

“ Kuna taasisi tunazidaiwa hadi bili ya Sh milioni mbili, Milioni moja, kushindwa kulipa hizi bili kwa wakati inatupa wakati mgumu katika kutekeleza majukumu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na ufasaha,” amesema Asha.

Kutokana na hali hiyo, Simalenga, akaagiza taasisi zote ambazo zinadaiwa zikatiwe huduma ya maji, na ikiwa zitakatiwa huduma hiyo zitatakiwa kwenda kwake kujieleza kwa nini zimekatiwa huduma hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button