MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ametoa elimu katika makazi ya wananchi, vijiwe vya boda boda, bajaji na masoko juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la mkazi na kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27.
DC Mpogole ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ilala ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala kufanya msako wa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani ndani ya siku mbili wenye sifa za kujiandikisha kwenye vituo vyao lakini hawakufanya hivyo
Mpogolo ameanza kutoa elimu hiyo leo baada ya kuanza ziara yake ya kata kwa kata na kuanza katika eneo la makutano ya barabara mataa ya kamata kwa kuelimisha Shirikisho la Vyama vya Bodaboda na bajaji pamoja na wasafiri wengine wa vyombo vya moto.
Amesema ni muhimu kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa wananchi wote wenye sifa kuanzia miaka 18 na kuendelea, mkazi halali wa mtaa huo, mwenye akili timamu ana haki ya kujiandikisha na kupiga kura.
“Umuhimu wa zoezi ili ni mkubwa kwa wananchi wote wenye sifa kujua uchaguzi wa mitaa unawahusu kuchagua viongozi wenu wa mitaa mnaokuwa nao katika makazi yenu na kusaidia kutatua kero zenu za kijamii,” amesema Mpogolo.
Ameongeza kuwa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi utawasaidia kupata viongozi bora, wanaosoma mapato na matumizi, wanaofanya mikutano na kusimamia ulinzi na usalama katika mitaa yao.
Aidha Mpogolo ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi kuwa Halmashauri ya Jiji ina zaidi ya bilioni 11 za kuwakopesha makundi ya bodaboda na bajaji au mmoja mmoja mikopo ambayo kwa sasa imeongezwa sifa kutoka umri wa miaka 35 hadi 45 tofauti na mikopo ya awali ilivyokua.
Akizungumzia suala la barabara ya Kitunda, kivule hadi Msongola amewahakikishia wananchi, wafanyabiashara, bodaboda na bajaji barabara hiyo imeshapata mkandarasi na mkataba wa ujenzi huo utashuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Serikali za Mikoa na Mitaa (TAMISEMI),Mohamed Mchengerwa wakati wowote kuanzia sasa.
Barabara ambayo itajengwa katika kiwango cha lami, mifereji, taa za barabarani na kuwa katika viwango vya kisasa ili kumaliza changamoto ya muda mrefu kwa wakazi wa kata ya kitunda, kivule na msongola.
Mpogolo amesema maendeleo ya wananchi katika sekta ya elimu, afya, miundombinu, na maji yanaanzia serikali za mitaa.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi kupitia kwa mratibu wake, SP Kasira kwa niaba ya kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es salaam amewahakikishia wananchi jeshi la polisi liko makini kuhakikisha ulinzi na usalama wakati wa kipindi cha kujiandikisha na kupiga kura unakuwa wa kutosha.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Bodaboda na Bajaji, Hussein Chanje ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuwasaidia maofisa usafirishaji kutambulika rasmi, kuingia mjini na kuongeza umri wa kuchukua mikopo kutoka miaka 35 hadi 45 hali inayofanya wafanye kazi zao kwa amani.
Umoja huo kupitia mwenyekiti wao wamehakikisha kushiriki vilivyo kujiandikisha na kupiga kura pamoja na kuhamasisha makundi mengine.
Huu ni mwendelezo wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo kuhamasisha zoezi la kujiandikisha na kupiga kura ambalo alilianzia mapema katika kata zote 36 za ilala, vijiwe vya kahawa, magazeti, michezo na kuendelea katika masoko, vijiwe vya bajaji, bodaboda, babalishe na mamalishe.
Comments are closed.