DC Ilala awataka vijana kudumisha amani, umoja

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka vijana kudumisha amani, umoja na mshikamano na kuwa wazalendo katika kudumisha demokrasia na kushiriki katika chaguzi kwa kupiga kura kwenye chaguzi za mitaa, vijiji na vitongoji.

Lengo likiwa ni kumuenzi Baba wa Taifa Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwani amekua kiongozi wa kuonesha mfano mzuri wa demokrasia haswa kwa kukubali uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 nchini.

Akizungumza na HabariLeo, Mpogolo amesema hayo leo Oktoba 14,2024 katika mahojiano maalum juu ya maadhimisho ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Amesema kuanzisha mfumo wa vyama vingi na kukubali kwake kung’atuka katika madaraka ni demokrasia tosha jambo ambalo si lakawaida kwa baadhi ya viongozi waliopigania uhuru wa nchi zao.

Ili kumuenzi Mwalimu Nyerere na kuendelea kumkumbuka ni vema vijana wa Tanzania kudumisha amani, umoja, mshikamano na kuwa wazalendo kwa taifa letu,” amesema Mpogolo.

Ameeleza kuwa miaka 25 ya kifo cha Mwalimu vijana wanatakiwa kujifunza maisha ya mwalimu Nyerere aliyependa Utu, kujifunza na kutosheka katika madaraka hali iliyomjengea heshima ya kisiasa nchini, barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Amesisitiza kitendo cha mwalimu Nyerere kuaminiwa na wazee na chama cha Tanu kuongoza Watanganyika kutafuta Uhuru ni kutokana na heshima, busara na unyenyekevu licha ya elimu yake alikubali kutumwa kusaidia nchi yake.

Mpogolo amesema Hayati Mwalimu Nyerere amekua na mchango mkubwa kuhakikisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar unafanikiwa kwa kushirikiana na aliyekua Rais wa Zanzibar Hayati Shekhe Abeid Amani Karume, muungano ambao hadi sasa unaendelea kudumishwa.

Ameongeza jambo ambalo Watanzania wataendelea kumkumbuka Mwalimu Julius Nyerere ni kuwacha katika misingi ya umoja, amani, upendo na mshikamano pamoja na kukemea suala la udini, ukabila na ukanda katika Taifa.

pia amesema licha ya ndoto kubwa ya Nyerere ya kutamani Bara la Afrika kuungana bado Watanzania wanaona mchango wake wa kuunda umoja wa nchi za Afrika mashariki unaendelezwa.

Mpogolo ameeleza alama aliyoacha Mwalimu Nyerere ni kubwa maeneo mbalimbali nje ya Tanzania kwa nchi zilizosaidiwa na Mwalimu Nyerere kupata uhuru ikiwemo Msumbiji, Afrika Kusini, Angola na Namibia.

Amebainisha kuwa hii ni kumbukizi ya miaka 25 ya Mwalimu Nyerere na bado watanzania wanashuhudia Marais wa awamu zote wakiendelea kulinda tunu za Taifa la Tanzania toka kifo chake kilipotokea toka kipindi cha awamu ya tatu chini ya hayati Benjamin Mkapa, awamu ya nne ya Jakaya Kikwete, awamu ya tano ya Hayati John Magufuli hadi sasa awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Habari Zifananazo

Back to top button