TANGA; MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Japhari Kubecha amefanya ziara Kata ya Manolo wilayani humo kutatua changamoto za wananchi waishio katika kata hiyo.
Taarifa ya DC Kubecha leo imeeleza kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa ziara ya Kliniki Tatua Kero inayolenga kuskiliza na kutatua kero za wananchi wa Lushoto.
“Nimekagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Shule ya Sekondari Manolo kwa majengo ya madarasa, Zahanati ya Kata ya Manola kwa jengo la operesheni ambazo ni nguvu za nchi na baada ya hapo kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za muda mrefu ndani ya kata,” amesema DC Kubecha.
DC Kubecha amesema ni muda mrefu umepita hakuna Mkuu wa Wilaya ambaye aliwahi kutembelea katika kata hiyo kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi. Ameahidi kufika katika kata na vijiji vyote kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Katika ziara hiyo DC Kubecha aliambatana na wakuu mbalimbali wa taasisi na idara pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, diwani na viongozi mbalimbali Kata ya Manolo.