DC Mvomero akemea tabia ya kuwadhuru Tembo
MKUU wa Wilaya ya Mvomero , mkoani Morogoro, Judith Nguli amekemea tabia ya wananchi wa wilaya hiyo kuwajeruhi wanyamapori hasa tembo kwani vitendo hivyo huamsha hasira kwa wanyama hao na hatimaye kuwaletea madhara kwenye maeneo yao.
Nguli amesema hayo Mei 19, 2023 wilayani humo wakati akifungua warsha ya kujadili utatuzi wa changamoto ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu inayoikabili Wilaya hiyo, warsha iliyoratibiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
“Nimepata taarifa kwamba kuna watu wanachokoza wanyama, mtu anajeruhi tembo, tembo ukishamjeruhi tayari anakuwa na hasira lazima asumbue hicho Kijiji kwasababu ana maumivu ” amesema Nguli
“Nimepata taarifa kuna baadhi ya tembo wanakutwa wakiwa na madonda, hata wakimkamata wanakuta tayari anavuja usaha, sasa tembo wa namna hii haiwezi kuwa rahisi kumzuia lazima atakufanyia fujo kwasababu ana maumivu” amesisitiza mkuu wa wilaya
Mkuu wa wilaya amekemea vitendo vya wananchi kufanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa hifadhi kama vile kilimo jambo ambalo linawafanya wanyamapori hao hasa tembo kuharibu mazao yao.
“Tunaona kabisa hifadhi imepakana na eneo la kijiji na mtu analima pembeni hii ni Changamoto kwa sababu yule mnyama akitoka tu anakumbana na hilo shamba, lazima aliathiri kwa sababu mnyama ni mnyama tu hana akili za kujua hili ni shamba nilikwepe” amesema Nguli
Naye Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Mlage Kabange amesema tathmini iliyofanywa na Mamlaka katika maeneo mbalimbali nchini imebaini kuwa watu wengi wanaopata madhara yanayotokana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu hususan tembo yanatokea Wakati wa alfajiri na usiku.
Hivyo ametoa rai kwa wananchi kuepuka kufanya matembezi yasiyo ya lazima nyakati za usiku na alfajiri.
Kabange amesema katika Kukabiliana na changamoto hiyo, Mamlaka imejenga kituo cha askari kwa ajili ya muitikio wa haraka ili kuweza kuwadhibiti Wanyama Wakali na Waharibifu kilichopo katika Kijiji Cha Sangasanga wilayani Mvomero.
Hivyo amewaomba viongozi wa Kijiji hicho kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza wananchi kukutumia kituo hicho kwa kutoa taarifa za matukio ya uvamizi wa Wanyama hao.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Mvomero, Jonas Van Zeeland ameziomba mamlaka zinazohusika na Wanyamapori hususan TAWA kuwavuna tembo kwa lengo la kuwapunguza ili kuwapunguzia wananchi adha wanayokumbana nayo.
Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali ambapo ilihusisha viongozi mbalimbali katika Wilaya hiyo wakiwemo wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, madiwani wa kata, wenyeviti na watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, wawakilishi wa wazee kutoka katika Wilaya ya Mvomero
.