KUELEKEA Uchaguzi wa Serikali za M itaa utakaofanyika Novemba 27,2024, Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, Kanali Michael Mtenjele amewasisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani.
Msisitizo huo umetolewa wakati wa kikao cha kutoa maelekezo ya uchaguzi huo kilichofanyika wilayani humo na kwamba katika kipindi chote cha uchaguzi ni muhimu kuzingatia amani, utulivu na kuepuka kutumia kigezo cha uchaguzi kwa ajili ya kuhatarisha amani iliyopo.
“Hatutakuwa tuko tayari kuona mtu yoyote anahatarisha usalama na amani katika eneo letu,lengo tufanye uchaguzi ulio na amani na utulivu kila mtu aweze kutekeleza wajibu wake na haki yake ya kidemoklasia mpaka hapo tutakapopata viongozi baada ya tarehe 27,2024,”amesema Mtenjele.
Kwa upande wao viongozi wa vyama pinzani kwenye halmashauri hiyo ikiwemo Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Hamisi Bakari ameomba uchaguzi huo uwe wa uwazi na haki ili amani iendelee kuwepo kwani hawawezi kudai amani bila kutenda haki.
Akitoa maelekezo kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi huo, Msimamizi wa uchaguzi wilayani humo, DCI Mariamu Mwanzalima amewahimiza wananchi katika wilaya hiyo kujitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wakazi wote wanaotaka kugombea.
Aidha amewataka wananchi wanaotaka kugombea nafasi hizo za uongozi ni wale wenye umri kuanzia miaka 21 au zaidi ikiwemo nafasi ya mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji.
Amesema kuanzia Novemba 1 hadi 7,2024 ni tarehe ya kuchukua na kurudisha fomu kwa watia nia ya kugombea ambapo uteuzi wa wagombea utafanyika Novemba 8 mwaka huu siku moja baada ya kukamilika kwa zoezi la kurudisha fomu.
Hata hivyo kwa mujibu wa kanuni zoezi la uandikishaji kwenye daftari la kudumu la mpiga kura litafanyika Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu katika vituo
vilivyopangwa huku wakazi wenye sifa za kupiga kura ni kuanzia umri wa miaka 18 au zaidi.