DC wa Monduli atangaza kugombea ubunge Isimani

IRINGA: Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea ubunge katika Jimbo la Isimani, Mkoa wa Iringa, kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Aidha katika tangazo lake hilo,DC Kiswaga amemtaka mbunge wa sasa William Lukuvi, kutekeleza kauli yake ya kutogombea tena kama alivyowahi kutamka hadharani na katika vikao vya ndani vya chama.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Lumilo Hotel, Manispaa ya Iringa, Kiswaga amesema uamuzi huo umetokana na msukumo mkubwa kutoka kwa wananchi wa Isimani wanaotaka mabadiliko ya uongozi baada ya zaidi ya miaka 30 ya utumishi wa Lukuvi kama mbunge wa jimbo hilo.

“Mimi sijatumwa na Rais kama wengine wanavyojinadi, bali ninakuja kwa nia ya dhati inayotokana na umoja wa wana-Isimani wanaotaka mwelekeo mpya wa maendeleo,” amesema Kiswaga mbele ya waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa Kiswaga, Lukuvi aliwahi kumpa hakikisho kuwa hatawania tena nafasi hiyo.

CCM yaweka ukomo ubunge, udiwani Viti Maalumu

Amesema kuwa mwaka 2022 walikutana maeneo ya Shoppers Plaza, jijini Dodoma, ambapo Lukuvi alitamka wazi kuwa hana mpango wa kugombea tena na yuko tayari kuwaachia wengine kukamilisha kazi za maendeleo alizozianzisha.

“Kauli hiyo aliitoa pia wakati wa kampeni za mwaka 2020 na kwenye vikao vya ndani ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo ni vyema akaheshimu maneno yake mwenyewe,” aliongeza Kiswaga.

Kiswaga pia alieleza hofu yake juu ya kile alichokiita mazingira ya vitisho dhidi ya wananchi na wagombea wengine ndani ya jimbo hilo.

Mbunge Lukuvi amekuwa akihudumu kama mbunge wa Isimani tangu miaka ya 1990 na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Kiswaga anasema ni wakati sasa kwa jimbo hilo kupata kiongozi mpya atakayeleta kasi mpya ya maendeleo.

“Uongozi si urithi. Kwa kuwa alitamka hadharani kuwa hatagombea tena, ni wakati wa kutekeleza ahadi hiyo na kuacha wengine wachukue kijiti,” alisisitiza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button