DCEA Kaskazini watoa elimu udhibiti dawa za kulevya

ARUSHA: MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa Za Kulevya (DCEA) Kanda yaa Kaskazini kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Same katika Mkoa wa Kilimanjaro wametoa elimu na kuunda mikakati ya pamoja kudhibiti dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Jamii kutoka DCEA, Shabani Miraji amesema lengo ni kushirikisha viongozi hao ni kuhamasisha mazao mbadala katika kukabiliana na kilimo cha dawa za kukevya aina ya mirungi katika Kata za Vudee, Tae, Gavao Saweni pamoja na maeneo mengine.
Naye Ofisa Sheria, Benson Mwaitenda amesema mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na washiriki zaidi ya 80 imewahusisha viongozi kutoka kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Same, madiwani, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya same, watendaji ngazi ya kata, vijiji na vitongoji kutoka Kata za Vudee, Tae na Gavao Saweni ambapo mgeni rasmi katika mafunzo hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Same ,Kasilda Mgeni.
Mwaitenda amesema mafunzo hayo yameshirikisha taasisi za serikali kutoka DCEA, Sekretariati ya Maadili ya Viongozi Wa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na wataalamu kutoka Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same.
Aidha, Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Saweni iliyopo Kata ya Gavao Saweni-Same zaidi ya 130 walipatiwa elimu kinga dhidi ya dawa za kulevya, rushwa na maadili ambapo pamoja elimu hiyo waliyoipata lakini pia walihamasishwa kushirikiana na DCEA kwa kuwafichua wahalifu wa dawa za kulevya katika maeneo yao kwa kupiga simu ya bure 119.