DCEA yabaini biskuti zilizochanganywa na bangi Dar

DAR ES SALAAM; MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imebaini uwepo wa kiwanda cha kutengeneza biskuti zilizochanganywa na bangi katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam.

Pia, imekamata kilo 423.54 za bangi iliyosindikwa maarufu kama Skanka.

Akizungumza leo Novemba 8, 2023 jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema wamekamata Skanka baada ya kufanyika operesheni maalum zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi.

Amefafanua kilo 158.54 zilikamatwa eneo la Kigamboni na Kawe jijini Dar es Salaam zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mabegi ya nguo tayari kwa kusafirishwa.

“Kilo 265 zilikamatwa katika matukio tofauti mikoa ya nyanda za juu Kusini zikiwa zimefichwa ndani ya magari kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine ikiwemo maboksi yenye matunda aina ya Apples zikisafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam,”amesema Lyimo

Amesema, Mamlaka hiyo imekata watu wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti kwa kuchanganya na Skanka katika eneo la Kawe huku akifafanua katika tukio hilo watuhumiwa walikutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga skanka na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi.

Aidha, Lyimo amesema DCEA imebaini maeneo yanayotumika kama masoko ya kusambaza na kuuza Skanka kwenye fukwe ya Bahari ha Hindi.

“Kutokana na operesheni hizo watu 16 wamekamatwa ambapo kati yao sita wamefikishwa mahakamani na 10 watafikishwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika,”amesema.

Akifafanua kuhusu Skanka( Skunk) amesema ni jina la mtaani linaloitambulisha aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu ikilinganishwa na bangi ya kawaida.

Ameongeza dawa hiyo ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto ambapo asilimia 75 ni bangi aina ya Sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya Indica.

“Kiwango cha sumu kilichopo kwenye sanka ni zaidi ya asilimia 45 ukilinganisha na bangi ya kawaida ambayo kiwango chake cha sumu ni kati ya asilimia 3 mpaka 10.

“Hivyo Skanka ina madhara makubwa zaidi kwa mtumiaji ikiwemo kuamsha na kuzidisha magonjwa ya afya ya akili kwa haraka.Imebainika kuwa watu wasiowaaminifu huchanganya sanka kwenye vyakula kama vile biskuti, keki, jamu , sharubati , tomato souce pia kwenye sigara na shisha.

” Lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha uuzwaji wa dawa hizo kwa kuficha na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto, “amesema.

Lyimo amesema wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wanapaswa kuwa makini na vyakula hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button