DCEA yataka ushiriki wa vijana kudhibiti dawa za kulevya

ARUSHA: Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amewataka vijana kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuelimisha jamii, kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuzuia matumizi ya dawa hizo.
Lyimo ametoa kauli hiyo wakati akifunga Jukwaa la Vijana la Afrika Mashariki na Kati la Kupambana na Dawa za Kulevya (EAYFD) lililofanyika kwa siku tatu jijini Arusha.
Jukwaa hilo liliwakutanisha vijana zaidi ya 200 kutoka Tanzania, Zanzibar, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini, Somalia, Malawi, Mauritania na Afrika Kusini.

Amesema jukwaa hilo limekuwa fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa kuwajengea vijana uelewa, maarifa na mtandao wa pamoja utakaowawezesha kuunganisha nguvu katika kupambana na changamoto ya dawa za kulevya inayozidi kuathiri jamii nyingi duniani.

“Jukwaa hili ni chachu ya mabadiliko. Limewakutanisha vijana kutoka mataifa mbalimbali na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya,tunaamini watakaporejea katika jamii zao watakuwa sehemu muhimu ya suluhisho la tatizo hili,”amesema.

Ameongeza kuwa tatizo la dawa za kulevya limeendelea kuvuka mipaka ya mataifa na kuwa tishio kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kati pamoja na taasisi mbalimbali ili kudhibiti uingizaji, usafirishaji na usambazaji wa dawa hizo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Jukwaa hilo, Halima Omar, amesema kongamano hilo limewawezesha vijana kubadilishana uzoefu na kupata ujuzi kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya, pamoja na kujifunza namna ya kushiriki kikamilifu katika kampeni za uhamasishaji ndani ya jamii zao.

Amesema kupitia mafunzo, mijadala na kubadilishana uzoefu, vijana wamejengewa uwezo wa kuwa sehemu ya viongozi wa mabadiliko katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya katika ngazi ya jamii, taifa na kanda.
Jukwaa hilo la vijana liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya DCEA Tanzania na wadau mbalimbali wakiwemo Blue Cross Tanzania, Blue Cross Kenya,International Federation Green Crescent pamoja na wadau wengine.



