DED Kibaha, Ifakara wasimamishwa kazi

DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amewasimamisha kazi Wakurugenzii wawili wa Halmashauri kuanzia Novemba 20, 2023 ili kupisha uchunguzi.

Wakurugenzi hao ni, Butamo Nuru Ndalahwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro, Lena Martin Nkaya.

Mchengerwa, amechukua hatua hiyo baada ya kupokea taarifa ya awali ya timu iliyoundwa kuchunguza tuhuma za wakurugenzi hao kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo katika halmashauri zao kwa nyakati tofauti.

Advertisement

Timu hiyo iliyoundwa na Katibu Mkuu kwa maelekezo ya Waziri Mchengerwa imebaini mapungufu ikiwemo kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo.

Uamuzi huo wa kuwasimamisha kazi umezingatia Kanuni ya 37 (1) na 38 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 ili kupisha uchunguzi wa kina.

Aidha amewasisitiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo.

Mchengerwa ameendelea kusisitiza kuwa hatasita kuchukua hatua stahiki kwa atakayethibitika kutenda kinyume.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *