DODOMA – Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema deni la taifa limeongezeka na kufikia Sh trilioni 91.7 hadi Machi 2024 ikilinganishwa na Sh trilioni 77 zilizokuwa mwaka jana ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.1
“Ongezeko la deni lilitokana na Serikali kuendelea kupokea fedha za mikopo ya zamani na mipya kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji,” Prof. Mkumbo ameliambia Bunge mjini Dodoma leo Juni 13.
Taarifa ya serikali inaonesha kuwa deni la ndani lilikuwa Sh trilioni 30.7 na deni la nje lilikuwa Sh trilioni 60.9. Hadi Machi 2024, benki za biashara ziliongoza kwa kuhodhi asilimia 42.0 ya deni la ndani ikilinganishwa na asilimia 34.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023. Aidha, mifuko ya jamii ilihodhi asilimia 33.9 ikifuatiwa na watu binafsi asilimia 11.3 na kampuni za bima asilimia 7.6.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji amefafanua kuwa ongezeko la deni lilichangiwa na kupanda kwa viwango vya kubadilisha fedha pamoja na kuongezeka kwa riba kwenye mikopo ya nje ambayo riba zake hutegemea mabadiliko ya hali ya soko.
Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Serikali ilikopa jumla ya Sh triliono 4.28 kutoka soko la ndani, sawa na asilimia 88.5 ya lengo la mwaka 2023/24.
SOMA: Serikali: Gharama za manunuzi zilishuka 2023
Kati ya kiasi kilichokopwa, Sh trilioni 2.7 zilitumika kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zilizoiva na Sh trilioni 1.55 zilitumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Taarifa ya Prof Mkumbo ilionesha kuwa Serikali ilikopa jumla ya Sh trilioni 1.56 kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Kiasi kilichokopwa ni sawa na asilimia 74.5 ya shilingi bilioni 2,100.5 ambazo Serikali ilipanga kukopa katika mwaka 2023/24,” amesema.
Hata hivyo, serikali imesema matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa Deni iliyofanyika Desemba 2023 yalionesha kuwa deni ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
Tathmini hiyo hufanyika kwa kuzingatia vigezo vya uhimilivu ambavyo ni uwiano wa deni halisi kwa Pato la Taifa, uwiano wa deni halisi kwa malipo ya nje na uwiano wa malipo ya deni kwa mapato ya ndani na mapato yatokanayo na mauzo ya nje.
Viashiria vya deni vilionesha kuwa kwa mwaka 2023/24: thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 20.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 114.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180; ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato yatokanayo na mauzo ya nje ni asilimia 11.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 15; na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani ni asilimia 11.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 18.