Serikali: Gharama za manunuzi zilishuka 2023

DODOMA – Gharama za manunuzi nchini Tanzania zilipungua kwa wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 4.3 mwaka 2022, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo ameliambia Bunge mjini Dodoma.

Taarifa rasmi ya serikali imeonesha Mfumuko wa bei kwa tabaka la kipato cha chini uliongezeka hadi asilimia 5.2 mwaka 2023 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 kutokana na ongezeko kubwa la bei katika makundi ya burudani, michezo na utamaduni kwa asilimia 13.8, vyakula na vinywaji baridi kwa asilimia 9.8 pamoja na afya kwa asilimia 9.1

Akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023, Prof Mkumbo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kwa jumla kulichangiwa na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuimarika kwa upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani na nchi jirani pamoja na kuimarika kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. 

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, Kiwango cha mfumuko wa bei kipo ndani ya lengo la nchi la muda wa kati (asilimia 3.0 – 5.0) na kinakidhi vigezo vya mtangamano wa kiuchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa asilimia isiyozidi 8.0 na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika wa asilimia 3.0 – 7. 

Ingawa wastani wa gharama ulikuwa chini, kundi la chakula na vinywaji baridi lilishuhudia mfumuko wa bei mkubwa zaidi wa wastani wa asilimia 6.8 ikilinganishwa na makundi mengine.

Kiwango hicho kilikuwa ni kidogo ikilinganishwa na asilimia 7.3 ya mwaka 2022. Prof. Mkumbo amesema mabadiliko hayo yalitokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa chakula nchini ikiwemo, kutoa ruzuku ya mbolea pamoja na kujenga na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua katika uzalishaji wa mazao ya chakula. 

SOMA: Uchumi wa Tanzania wakua kwa asilimia 5.4

“Kundi la huduma za fedha na bima lilikuwa na mfumuko wa bei mdogo zaidi wa wastani wa asilimia 0.1 mwaka 2023 kama ilivyokuwa mwaka 2022,” Waziri Mkumbo amesema. 

Kundi la makazi, maji, umeme, gesi na nishati nyingine lilifuatia kwa kuwa na mfumuko wa bei mdogo wa wastani wa asilimia 1.6 mwaka 2023 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.6 mwaka 2022.

Mfumuko wa bei wa msingi (core inflation) ulipungua hadi wastani wa asilimia 2.3 mwaka 2023 kutoka asilimia 3.0 mwaka 2022. Aidha, Mfumuko wa bei kwa kundi la nishati, mafuta na ankara za maji ulikuwa asilimia 2.3 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 9.1 mwaka 2022. 

“Hii ilichangiwa na kupungua kwa kasi ya ongezeko la bei ya bidhaa za petroli katika soko la dunia. Vile vile, mfumuko wa bei za bidhaa na huduma ulikuwa wastani wa asilimia 4.6 na asilimia 2.5 mwaka 2023, kutoka asilimia 5.3 na asilimia 2.8 mtawalia mwaka 2022,” Waziri Mkumbo alifafanua.

Vilevile serikali imesema mfumuko wa bei kwa matabaka ya kipato cha kati na juu ulipungua hadi asilimia 4.9 na asilimia 2.5 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 5.8 na asilimia 3.8, mtawalia mwaka 2022. 

Habari Zifananazo

Back to top button