Serikali yaendelea kulinda ajira viwandani

DAR ES SALAAM: Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kulinda ajira zilizopo na kuzalisha ajira mpya kupitia viwanda na biashara kwa manufaa ya Watanzania na taifa.

Hayo ameyasema Mei 08, 2026 jijini Dar es Salaam alipotembelea Kiwanda cha Nguo cha Tooku Garments kilichopo Ubungo External na kubainisha kuwa ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali kujiridhisha na utendaji wa viwanda nchini, na kupanua wigo wa biashara.

Amesema kiwanda hicho kimeajiri takribani vijana 7,000, ambapo asilimia 75 ni wanawake huku asilimia 60 ikiwa ni vijana walio chini ya umri wa miaka 30.
Aidha, Waziri Kapinga amesisitiza kuwa Serikali inachukua hatua muhimu kutatua changamoto zinazokikabili kiwanda hicho na viwanda vingine nchini, ili kuboresha mazingira ya biashara.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TOOKU GARMENTS Borja Trenor Casanova- Genaral Manager amesema kuwa hakuna shaka, kiwanda hicho ndio wanufaika wakuu wa AGOA nchini, wakiwa wasafirishaji wakubwa wa mavazi kwenda Marekani.

Amesema hivi sasa wanashinikiza AGOA iongezwe kwa miaka 10 hadi 20 ili kukuza uwekezaji nchini ambapo kiwa mpango huo utafanikiwa, wanalenga kufikisha wafanyakazi 30,000.



