Uchumi wa Tanzania wakua kwa asilimia 5.4

Serikali imesema mikakati ya kukabiliana na athari za vita katika eneo la Ukraine pamoja na uwekezaji katika sekta za kilimo, nishati, maji, ujenzi, madini na usafirishaji ilichochea kukuza uchumi kwa asilimia 5.4 mwaka 2024 kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo

DODOMA – Serikali imesema mikakati ya kukabiliana na athari za vita katika eneo la Ukraine pamoja na uwekezaji katika sekta za kilimo, nishati, maji, ujenzi, madini na usafirishaji ilichochea kukuza uchumi kwa asilimia 5.4 mwaka 2024 kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023.

Kiwango hiki ni juu kidogo ya wastani wa asilimia 4.4 uliotazamiwa mwaka 2023 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na asilimia 3.8 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema katika Taarifa yake ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 aliyoitoa Bungeni mjini Dodoma leo Juni 13 kuwa Pato halisi la Taifa lilifikia Sh bilioni 148,399.76 mwaka 2023 kutoka Sh bilioni 141,247.19 mwaka 2022.

Advertisement

“Ukuaji huo ulichangiwa na: jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo mikakati ya kukabiliana na athari za vita kati ya Ukraine na Urusi pamoja na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu na usafirishaji,” alisema.

Maeneo mengine kwa mujibu wa Waziri wa Mipango ni kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi. 

Hata hivyo, kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa cha asilimia 5.1 mwaka 2023 kipo chini ya lengo la mwaka la asilimia 5.2. 

SOMA: Zanzibar kuwasilisha bajeti ya tril 4/

Kwa mujibu wa Mkumbo, hali hiyo ilitokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji katika baadhi ya sekta; mabadiliko ya tabianchi yaliyoathiri uzalishaji katika sekta ya kilimo kwa baadhi ya maeneo nchini na kuharibu miundombinu ikiwemo madaraja na barabara.

Prof. Mkumbo amesema pamoja na hatua zilizochukuliwa na nchi zilizoendelea katika kukabiliana na mfumuko wa bei ulio sababisha kuongezeka kwa gharama za mikopo kutoka masoko ya kimataifa ya fedha pia uliathiri shughuli za uzalishaji.

Tathimini ya Mwenendo wa Ukuaji wa Uchumi na Mchango wa Ukuaji katika kila Robo Mwaka katika kipindi cha 2019 na 2023 inaonesha kuwa uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.9 mwaka 2019, asilimia 4.5 (2020), asilimia 4.8 (2021), asilimia 4.7 mwaka 2022 na asilimia 5.1 mwaka 2023.

Prof. Mkumbo alifafanua kuwa sekta ya kilimo ilikuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye Pato la Taifa ikichangia asilimia 26.5. Sekta zingine zilizochangia zaidi ni pamoja na Ujenzi (asilimia 13.2), madini (asilimia 9), biashara na matengenezo (asilimia 8.3), usafirishaji (asilimia 7.2) na viwanda asilimia 7.

Kwa mujibu wa Mkumbo, Sekta ya Sanaa na Burudani bado ziliongoza kwa kuwa na kasi ya ukuaji mwaka 2023 zikikuwa kwa asilimia 17.7 ikifuatiwa na sekta ya fedha na bima asilimia 12.2 na madini asilimia 11.3.

Malazi na huduma za chakula zilikua kwa asilimia 8.3 pamoja na sekta ya Habari na Mawasiliano zilizokua kwa asilimia 7.6