Dewji aipa neno TFF

“TFF wafanye jitihada, wachezaji wazuri wako wengi, bado chipukizi wako mashuleni kila mkoa waangalie namna ya kwenda kuvuna vipaji”
Azim Dewji

DAR ES SALAAM – MFADHILI wa zamani wa timu ya soka ya Simba, Azim Dewji amelishauri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufanya maandalizi ya michuano ya Afcon ya mwaka 2027 kwa kuanza kutafuta na kukuza vipaji vya mpira.

Amesema hatua hiyo itasaidia itakapofika michuano hiyo, Tanzania iwe na timu nzuri itakayofika hatua za juu badala ya kutolewa katika hatua za awali.

Dewji aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali ya nchi, ikiwemo mchezo wa soka.

Advertisement

Alisema amefurahishwa na mafanikio ya Tanzania katika viwango vya Fifa lakini anatamani kuona ikipanda zaidi na kwamba hatafurahishwa wala Watanzania hawatafurahi kuona Tanzania ndiyo mwenyeji wa michuano hiyo halafu watolewe katika hatua za awali.

“Timu ya taifa ni ya Watanzania wote kwa hiyo nitafurahi kama kiwango kitafika chini ya 75, ikipanda zaidi nitafurahi, nasema hivyo kwa sababu miaka miwili ijayo tutakuwa na Afcon, sitapendezwa kuona sisi ndiyo wenyeji halafu tunatolewa mzunguko wa kwanza, nataka angalau tuingie nane bora, tutakuwa tumeweka ushindi,” Alishauri TFF kuanza kuandaa timu sasa kwa kuvuna vipaji vilivyoko mafichoni, waviibue ili wakati utakapofika Tanzania iwe na timu nzuri.

SOMA: Yanga kujiuliza kwa Namungo leo

“TFF wafanye jitihada, wachezaji wazuri wako wengi, bado chipukizi wako mashuleni kila mkoa waangalie namna ya kwenda kuvuna vipaji baada ya miaka miwili kuwe na wachezaji ambao watapeperusha bendera ya nchi vizuri,” alisema.

Aidha, alisema amefurahi kuona timu ya Simba imeshinda lakini alitamani kuona inashinda zaidi kwa kuwa ushindi wa goli moja unaweza kurudishwa kwa urahisi. Septemba mwaka jana, Shirikisho la Soka barani Afrika ilizipa Kenya, Uganda na Tanzania haki ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Rais wa Caf, Patrice Motsepe alitangaza Zabuni ya Pamoja ya Afrika Mashariki kama mshindi wa haki za kuandaa bonanza la kwanza la kandanda la Afrika baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Caf mjini Cairo, Misri.