DAR ES SALAAM – YANGA leo itakuwa ugenini kuikabili Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa michezo miwili mfululizo ambapo ilifungwa na Tabora United 3-1 na kufungwa na Al Hilal kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa bao 1-0.
Hadi sasa Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic hajashinda mchezo tangu ajiunge na mabingwa hao watetezi, hivyo huo ndio mchezo utakaomfanya arudishe imani kwa mashabiki endapo watashinda.
Akizungumza kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic alisema anajua utakuwa mchezo mgumu kwa sababu Namungo ina wachezaji wazoefu lakini wao wanahitaji pointi tatu.
“Tuna mchezo mgumu na muhimu sana kesho (leo), katika maandalizi yetu kila kitu kipo vizuri, tunafahamu Namungo wana wachezaji wazoefu lakini sisi tupo hapa kutafuta pointi tatu.
“Kwa kweli ni jambo la kujivunia sana na nawashukuru mashabiki wa Yanga wanaotoka Dar es Salaam leo usiku na Wanayanga wote wanaokuja kuisapoti timu yetu, mimi na wachezaji tunapaswa kuwalipa furaha kwani wameonesha moyo na mapenzi ya dhati, tunajiandaa kuirejesha furaha yao,” alisema Ramovic.
Naye Denis Nkane alisema, “Sisi wachezaji tunatambua umuhimu wa pointi tatu, tumekaa chini na kuzungumza wapi kwa kuboresha, tunamsikiliza mwalimu na kujituma kwa dhati ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.
SOMA: Simba inaleta heshima kimataifa
“Mchezo wa kesho ni mgumu lakini tupo kwa ajili ya kupambana na kushinda na wapongeza wana Yanga kwa mapenzi wanayoonesha, hili ni deni kwetu mje kutusapoti kwani tupo hapa kwa ajili ya kushinda,” alisema Nkane.
Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza michezo 10 na Namungo inashika nafasi ya 13, ikiwa na pointi tisa katika michezo 11 iliyocheza