Dhahabu, nafaka, utalii vyapaisha mauzo nje

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema mauzo ya bidhaa na huduma nje yameongezeka.
Taarifa ya Tathmini ya Uchumi ya BoT kwa Septemba mwaka huu inaeleza ongezeko hili lilichangiwa zaidi na mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
BoT imeeleza mauzo hayo yaliongezeka kwa asilimia 15 hadi Dola za Marekani milioni 16,935.6 mwaka unaoishia
Agosti mwaka huu, ikilinganishwa na Dola milioni 14,720.3 katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Taarifa hiyo imeeleza mauzo ya bidhaa yalifikia Dola milioni 9,886.9, ikilinganishwa na Dola milioni 8,055.2 katika kipindi kama hicho mwaka ulioishia Agosti mwaka jana.
SOMA: Akiba ya dhahabu BoT yafikia tani 6
“Ongezeko hili lilichangiwa zaidi na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani, korosho, tumbaku na nafaka,” imeeleza BoT.
Ameongeza: “Mauzo ya dhahabu yaliongezeka kwa asilimia 35.5 hadi Dola za Marekani milioni 4,322.3 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 3,189.4. Ongezeko hili lilitokana na ongezeko la bei ya dhahabu katika soko la dunia.”
Taarifa imeeleza bidhaa asilia ziliongeka kwa asilimia 28.3 na kufikia Dola za Marekani milioni 1,411.7 ikichangiwa zaidi na mauzo ya korosho, tumbaku na kahawa, kutokana ongezeko la bei na uzalishaji.
BoT imeeleza mauzo ya nafaka yalifikia Dola za Marekani milioni 341.2 kutoka Dola za Marekani milioni 174.6, kutokana na ongezeko la mahitaji ya bidhaa hizo katika nchi jirani.
“Kwa mwezi mauzo yalifikia Dola za Marekani milioni 1,024.8 mwezi Agosti 2025, ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 922.4 mwezi Agosti 2024, ikichangiwa zaidi na mauzo ya dhahabu na tumbaku,” imeeleza
taarifa.
BoT imeeleza mapato ya huduma yaliongezeka na kufikia Dola za Marekani milioni 7,048.7 katika mwaka ulioishia Agosti 2025, ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 6,665.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.
“Ongezeko hili lilichangiwa zaidi na mapato ya utalii na usafirishaji. Mapato ya utalii yaliongezeka na kufikia Dola za Marekani milioni 3,875.4, ikiashiria kuimarika kwa shughuli za utalii. Idadi ya watalii iliongezeka hadi 2,287,377 kutoka 2,051,404,” imeeleza taarifa.
Makusanyo BoT imeeleza Julai mwaka huu makusanyo ya mapato ya serikali, yakijumuisha ya serikali za mitaa yalifikia Sh bilioni 2,911.6, sawa na asilimia 103 ya lengo.
Taarifa imeeleza kati ya kiasi hicho, serikali kuu ilikusanya Sh bilioni 2,777.6 ikijumuisha mapato ya kodi Sh bilioni 2,345.8 na mapato yasiyo ya kodi Sh bilioni 431.8.
“Makusanyo ya kodi ya mapato na ushuru wa forodha yalivuka lengo lililowekwa. Mafanikio haya ni matokeo ya uboreshaji mfumo wa ukusanyaji na usimamizi wa kodi na kuongezeka kwa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi,” imeeleza taarifa.
Sekta ya benki BoT imeeleza hali ya ukwasi katika sekta ya benki iliimarika na kiwango cha riba cha siku saba katika soko la fedha baina ya benki kiliendelea kuwa karibu na riba ya Benki Kuu ya asilimia 5.75.
Taarifa imeeleza mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kuchukua sehemu kubwa ya mikopo yote, ikiwa na asilimia 36 ikifuatiwa na biashara na kilimo zilizokuwa na asilimia 14.2 na asilimia 13.2, mtawalia.
“Shughuli za kilimo ziliendelea kuwa na ukuaji mkubwa wa mikopo ambapo Agosti 2025 ukuaji wa mikopo ulioelekezwa katika shughuli za kilimo ulifikia asilimia 30.1, ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 29.2 na mawasiliano na uchukuzi, asilimia 18.8,” imeeleza BoT.