Diogo Jota afariki kwa ajali

MSHAMBULIAJI wa mabingwa wa Ligi Kuu England, Diogo Jota amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika ajali ya gari akiwa na umri wa miaka 28.

Idara ya Ulinzi wa Kiraia ya Hispania imesema pia ndugu wa Jota, Andre Silva amefariki katika ajali hiyo iliyotokea katika Valladolid uliopo Jimbo la Zamora.

Andre mwenye umri wa miaka 26 pia alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya Penafiel inayoshiriki Ligi Daraja la pili.

Maafisa wa idara hiyo wamesema gari lao aina ya Lamborghini liliacha njia kutokana na kupasuka tairi wakati wakilipita gari lingine kisha kubiringika na kuwaka moto.

Wiki mbili zilizopita Jota alifunga ndoa na rafiki yake wa muda mrefu Rute Cardoso, ambapo wamepata watoto watatu.

Jota aliisaidia Liverpool kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita na pia alihusika Ureno ilipoishinda Hispania katika fainali ya kombe la Ligi ya Mataifa ya Ulaya mwezi uliopita.

“Shirikisho la Soka la Ureno (FPT) na wapenda soka kote Ureno wamepata mshtuko mkubwa kutokana na kifo cha mchezaji huyo,” amesema Mkuu wa FPT, Pedro Proenca.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button