Diwani Mutayoba atoa somo uchaguzi serikali za mtaa,vijiji

MISENYI, Kagera: KUELEKEA Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadae mwaka huu, Diwani wa Kata ya Kitobo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Willy Mutayoba amewaasa wananchi kuhakikisha hawakosei katika kupiga kura kupata wawakilishi kwani hilo linaweza kuwagharimu kwa miaka mitano mbele.

Akizungumza na mwandishi wetu juu ya maendeleo ya Kata ya Kitobo, Mutayoba amesema, katika mwaka wa fedha 2023/24 Kata ya Kitobo imekabidhiwa takribani Sh bilioni 2.5 ya mapato ya serikali kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi mkubwa wa maji kutoka msitu wa Kabwiru, ujengaji wa barabara za kisasa kilimita 19 na barabara ya michepuo katika maeneo ya Misheni-Taru road na Kashasha.

Mradi mwingine ni bwawa la uvunaji wa samaki kwa vijana fedha zilizotolewa na Mbunge takribani Sh bilioni 12 pamoja na mradi wa upandaji miche 2500 ya parachichi afya.

“Tumepokea zaidi ya Sh milioni 910 kwaajili ya utekelezaji wa mradi wa maji ulio chini ya Benki ya Dunia (WB),” amesema diwani huyo.

Amesema, mradi huo wa maji umeenea kata nzima na zaidi ya watu 350 wameshasambaziwa maji na utekelezaji huo unaendelea kuhakikisha kila mwananchi anasambaziwa maji.

“Kuna Kitongoji cha Bwaja na Lubumba ambapo wananchi wana changamoto ya maji. Tupo katika hatua ya kuchipusha maji kuhakikisha wananchi wote yanawafikia kwenye maeneo yao,” amesema.

Amesema katika maeneo ya kutolea huduma kwa wananchi kama shule na vituo vya afya usambazaji wa huduma ya maji na umeme unaendelea vizuri.

Mbali na mradi huo, amesema serikali imeahidi kata hiyo pia ihusishwe katika mradi wa maji unaoendeshwa na WB kutoka Ziwa Victoria ambao utatatua kabisa changamoto ya umeme.

Hata hivyo, Mutayoba amesema wanaendelea kufanya mawasiliano na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha vifaa vya kufungia maji kwa wananchi vinakuwa katika ubora na bei rafiki.

Diwani huyu anayepeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema Kata ya Kitobo ina vijiji vitano, vitongoji 17 ambavyo vyote vipo chini ya uongozi wa CCM.

Habari Zifananazo

Back to top button